TUME ya Mabadiliko ya Katiba imeombwa
kuhakikisha kuwa Katiba mpya inawekwa kipengele cha kupiga marufuku talaka
nchini.
Sambamba
na hilo, imependekezwa kuwa Katiba ikataze watumishi wa Marais, Mawaziri Wakuu
na wa Makamu wa Rais waliostaafu kuendelea kulipwa na serikali. Akitoa maoni
katika mkutano wa kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya katika Kata ya Mpitimbi,
wilayani Songea mkoani Ruvuma, Alandus Mpiyi (61) alisema watu wamekuwa
hawamheshimu Mungu kwa kupeana talaka ovyo. Mpiyi alisema kila kukicha kumekuwa
na talaka zinazozidi idadi ya watu wanaooana na hivyo heshima hiyo kupotea na
kupendekeza Katiba mpya iweke bayana amri ya kupiga marufuku talaka. Alipoulizwa
na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliyekuwepo
mkoani humo kwa tathimini ya mchakato kupitia sehemu ya Tume iliyoko mkoani
hapa kuwa dini zote zinatambua talaka iweje Katiba ipinge, Mpiyi alisema: “Hata
kama serikali inatambua hilo, ndio maana tuko hapa kutoa maoni ya Katiba mpya
si ya zamani, hao wanaotaka kuachana, walioanaje? Nani aliwalazimisha kuoana
mpaka sasa wanalazimisha kuachana, hakuna ruhusa hiyo, ipigwe marufuku kabisa”.
Alipendekeza iwekwe kwenye Katiba mpya ili kila dini, utamaduni na mtu yeyote
alazimike kuheshimu amri hiyo na kuifuata ili kuweka heshima kwa taifa. Kuhusu
kulipwa watumishi wa viongozi wa kuu wa serikali waliostaafu, wakiwemo
madereva, walinzi na watumishi wa ndani, Benedict Haule (28) alipendekeza kuwa
Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu waliostaafu, waondolewe malipo kwa watumishi
wao.
0 comments:
Post a Comment