MLEZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa mikoa
ya Njombe, Iringa na Mbeya, Thomas Nyimbo, ametangaza kujivua uanachama wa
chama hicho kwa madai ya kuchoshwa na siasa za ‘Umangimeza’ ndani ya vyama vya
siasa hapa nchini.
Nyimbo ambaye amewahi kuwa mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
kwa miaka 10 katika Jimbo la Njombe Magharibi kabla ya kukimbilia Chadema mwaka
2010, amesema hivi sasa atabaki kuwa mwanasiasa huru asiyefungamana na vyama.
Akitoa taarifa ya kuachana na siasa ndani ya vyama jana, Jijini
hapa, huku akiwa ameambatana na mkewe Mary Mwenga, alisema amechukua uamuzi huo
baada ya kuona siasa za kushabikia vyama hazina tija kwa watanzania walio wengi
na badala yake zinawanufaisha viongozi wachahe wanaojineemesha wao wenyewe kwa
kutumia jasho la wananchi.
Akifafanua zaidi alisema alichojiuzulu ni siasa za vyama, lakini
sio siasa, huku akitamba kuwa yeye alizaliwa akiwa ni mwanasiasa, kiongozi na
mtu ambaye mawazo yake yanahitajika kwa ajili ya maendeleo ya nchi yake, hivyo
atabaki kuwa mwanasiasa asiyekuwa na chama cha siasa.
Katika taarifa hiyo aliyoitoa kwa vyombo vya habari mithiri ya
Mhadhara, Nyimbo alitumia zaidi ya saa moja na nusu kuelezea mustakabali wa
taifa na vijana kutokana na vyama vya siasa kuelekea kuwatumbukiza kwenye
machafuko.
“Nimeachana na Chadema baada ya kubaini kuwa siasa za vyama havina
tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla na ni wakati huu sasa wa kuachana na
dhana ya vyama vya siasa vituandalie sera na tunahitaji sasa itungwe sera ya
kitaifa ambayo mgombe inabidi atueleze tukimchagua ataitekeleza vipi” alisema
Nyimbo.
Alisema hata nchi zenye wigo mpana wa Demokrasia kama Marekani
ambao hivi sasa wapo kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu huwezi kuwasikia wagombea
wake wakisifia vyama vyao, bali wanawaeleza wananchi wa Marekani watatekeleza
vipi sera ya nchi yao .
Alisema kuwa ikiwa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa
itakuruhusu mgombea huru, atakuwa tayari kugombea ubunge tena kwenye jimbo lake
la Njombe Magharibi, lakini kama katiba hiyo itazuia fursa hiyo hatogomea tena
wadhifa huo maisha yake yote.
Aliongeza kuwa baada ya kupatikana kwa katiba mpya, inabidi
itungwe sera ya Taifa itakayolindwa kisheria, ambayo kila chama
kitakachofanikiwa kuingia madarakani kilazimike kuifuata badala ya ilivyo sasa
vyama vinaogelea hovyo.
Alisema kuwa ndoto za kuwa mwanasiasa huru alikuwa nazo tangu
zamani, na ndiyo sababu katika mabango yake ya kuhamasisha achaguliwe wakati
akigombea ubunge kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alikuwa na kauli mbiu ya
‘Mtu kwanza, chama baadaye.
Alisema kuwa ikiwa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa
itakuruhusu mgombea huru, atakuwa tayari kugombea ubunge tena kwenye jimbo lake
la Njombe Magharibi, lakini kama katiba hiyo itazuia fursa hiyo hatogomea tena
wadhifa huo maisha yake yote.
“Nitapenda kushauriana na watanzania wanaopenda maendeleo ya
taifa letu nje ya mlolongo wa vyama, hivyo hata kama naipenda vipi Chadema,
nalazimika kuresighn (kujiuzulu) uanachama ili niweze kutimiza azma hiyo,”
alisema Nyimbo.
Kilicho mkimbiza Chadema.
Alisema ameamua kujiondoa ndani ya chama hicho baada ya kubaini
kuwa kinaenda kinyume na malengo yake kama kinavyojipambanua mbele za watu.
Alisema licha ya kuwaaminisha wananchi, hususani vijana kuwa
ndio chama chenye kuleta mabadiliko ya kweli,lakini viongozi wake wa daraja la
juu akiwataja Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa
wamekuwa wakijinufaisha binafsi.
Alisema viongozi hao pia wamekuwa si watu wa kushaurika ndani ya
chama hicho, lakini kibaya zaidi ni kuendesha siasa katika mfumo mbaya wa
kushawishi na kuaminisha bila kuwa na suluhisho (Mob Politics).
Alisema siasa za namna hiyo ni hatari kwa taifa kwa kuwa baada
ya kuungwa mkono kwa kiwango cha juu na kundi la vijana kwa imani ya
kukombolewa pale watakapofanikiwa kuingia madarakani na kushindwa kuwatimizia
kutazua vurugu.
Kuhusu CCM.
Nyimbo alidai kuwa chama hicho kinajimaliza chenyewe kutokana na
kuacha suala la rushwa kwenye chaguzi zake za ndani kuwa ndio kigezo muhimu cha
kuwapata viongozi wake.
Hata hivyo alisema ili tatizo hilo limalizike ni wananchi
wenyewe kuamua kuikataa rushwa kwa kupokea rushwa isiyoleta matunda kwani
wakifanya hivyo watakuwa wamemaliza tatizo hilo .
“Mfano wewe ukipokea rushwa na kuamua kufanya tofauti na
aliyekuhonga kwa kuwa baadaye atakuwa hajapata kile alichotaka kukinunua toka
kwako, unafikiri kesho atarudia”.
Vijana.
Amewataka vijana nchini kupigania maslahi yao kwa mtazamo hasi
wenye kuleta mstakabali mzuri wa Taifa, badala ya kufikiri kuwa mabadiliko ni
kuiondoa CCM madarakani na kuiweka Chadema.
Alisema kuna mambo mengi ya msingi ambayo kama vinana wanapaswa
kuwahoji viongozi waliowachagua kama wameyatekeleeza , ikiwemo kupigania katiba
mpya kuwa na sera ya inayoweza kuruhusu mgombea binafsi kwa kuwa huko wanaweza
kupata viongozi bora.
Kujiengua kwa Nyimbo linaweza kuwa ni pigo kubwa kwa Chadema,
kwani baada ya kujiunga na chama hicho mwaka 2010, alikuwa ni mlezi wa Chadema
kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, huku pia akiwa ni miongoni mwa wanasiasa
wenye mvuto na wahamasishaji wazuri wa Chadema katika mkoa mpya wa Njombe.
|
0 comments:
Post a Comment