MENEJA wa uwanja wa Sokoine uliopo jijini Mbeya
Modestus Mwaluka amesema maandalizi ya uwanja kwaajili ya ligi kuu ya Tanzania
bara yamekamilika.
Akizungumza na JAMII YANGU, Mwaluka amesema
kinachosubiriwa sasa ni kuanza kwa ligi hiyo lakini kwa upande wa maandalizi ya
uwanja hakuna la ziada tena katika maandalizi.
Amesema yapo maboresho makubwa yaliyofanyika katika
uwanja huo na sasa upo katika kiwango cha ubora unaofaa kwa michuano mikubwa
kama ligi kuu inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwanzoni mwa mwezi ujao.
Amesema miongoni mwa maeneo yaliyofanyiwa ukarabati
ni pamoja na eneo la kuchezea(Pich) ambalo limejazwa udongo na kuoteshwa nyasi
katika maeneo yaliyokuwa na mabonde hali ambayo awali ilikuwa ikisababisha
usumbufu kwa wachezaji wakiwa katika mechi husika.
Meneja huyo amesema kwa maboresho yaliyofanyika kwa
sasa uwanja uko katika hali nzuri na hata wachezaji wataona raha kuutumia
tofauti na awali.
Kwa upande wa masuala ya usalama,Mwaluka amesema kwa
sasa usalama wa wachezaji wawapo uwanjani,wale wa akiba pamoja na waamuzi na
wahusika wengine ni mkubwa kutokana na wigo uliopo ambao katika siku za mechi
ulinzi utaimarishwa zaidi ili mashabiki wasipate fursa ya kuingia eneo
lisilowahusu.
“Mpaka sasa hatujapata ratiba lakini kwa taarifa
tuilizonazo wakati wowote kuanzia leo itatoka.Kwa upande wetu kama wamiliki na
wasimamiaji wa uwanja tumekamilisha mambo yote muhimu ikiwemo uboreshaji wa
maeneo korofi.Tunachosubiri ni kuanza tu kwa ligi” amesema Mwaluka.
Hata hivyo baadhi ya wadau wa michezo jijini Mbeya
wakiwemo wanahabari wameshauri uongozi wa uwanja kwa kushirikiana na chama cha
soka mkoani Mbeya (MREFA) kuhakikisha unakuwepo utaratibu maalumu ambao
hautaruhusu mamluki kuvamia eneo la wanahabari.
Katika ligi kuu ya Tanzania bara msimu huu,mkoa wa
Mbeya na mingine iliyopo jirani itawakilishwa na timu ya Tanzania Prisons ya
jijini hapa iliyopata daraja baada ya kufanya vyema katika michuano ya ligi
daraja la kwanza iliyopita.
0 comments:
Post a Comment