SIMBA SC imetwaa ubingwa wa michuano mipya, BankABC Sup8R jioni
ya jana, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, baada ya kuifunga Mtibwa Sugar ya Morogoro
mabao 4-3, katika mchezo uliodumu kwa dakika 120.
Shujaa wa
Simba, alikuwa ni Christopher Edward ambaye alifunga mabao matatu peke
yake na kufikisha jumla ya mabao tisa, hivyo kujinyakulia tuzo ya ufungaji bora
wa michuano hiyo na kuzawadiwa Sh. Milioni 2. Hadi mapumziko, timu
hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba iliyotumia kikosi chake cha pili
kwenye michuano hiyo, Simba B ikitangulia kupata bao dakika ya 13, mfungaji
Christopher Edward aliyepokea pasi safi
ya Ramadhan Singano ‘Messi’. Mtibwa walisawazisha bao hilo kwa penalti dakika ya 32, mfungaji
Shaaban Kisiga ‘Malone’, baada ya Jamal Mnyate kuangushwa kwenye eneo la hatari
na Hassan Hatibu. Mnyate hakuweza kuendelea na mchezo baada ya pigo hilo na nafasi yake ikachukuliwa na Hassan
Seif. Kipindi
cha pili, Simba inayofundishwa na Suleiman Matola, ilirudi kwa kasi tena na
kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 54, Edward akiunganisha krosi maridhawa
ya Rashid Ismail. Dakika ya
57 Mtibwa Sugar walisawazisha bao hilo
kwa mpira wa adhabu nje kidogo ya eneo la penalti, ambalo lilipigwa na Shaaban
Kisiga ‘Malone’ na kumpita kipa Abuu Hashim, aliyepewa tuzo ya Mchezaji Bora wa
Mashindano (MVP) na kuzawadiwa Sh. Milioni 2.5.
Simba ilipata bao la tatu dakika
ya 66, safari hii akifunga Haroun Athumani, kabla ya Hassan Seif kuisawazishia
Mtibwa dakika ya 79 kwa mpira wa adhabu tena, uliompita kirahisi kipa mfupi
Abuu. Hadi
dakika 90 za mchezo huo zinamalizika, timu zote zilikuwa zimefungana mabao 3-3
na katika dakika 30 za nyingeza, Edward aliihakikishia Simba B Sh. Milioni 40
na Kombe la michuano hiyo mipya kwa bao lake safi dakika ya 112, akiunganisha
pasi ya Haroun.
Safari
hii, Watoto wa Matola hawakurudia kosa la kucheza rafu karibu na lango lao,
walitulia na kucheza soka ya kuonana kwa pasi nzuri za uhakika na kwenye
shambulizi wanabutua mpira, Mtibwa warushe na hadi kipyenga cha mwisho, Simba B
waliibuka vinara. Mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella
Mukangara alikabidhi Kombe na mfano wa Hundi, yenye thamani ya Sh. Milioni 40
kwa Nahodha wa Simba B, Hassan Hatibu, wakati wachezaji wa timu hiyo, kila
mmoja walipewa mfano wa Medali za Dhahabu. Mtibwa Sugar walipewa Hundi ya Sh.
Milioni 20 na mfano wa Medali za Fedha kila mmoja.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; Abuu Hashimu, William Lucian ‘Gallas,
Omary Salum/ Jesse Nyambo, Hassan Isihaka, Hassan Hatibu, Said Ndemla, Haroun
Athumani, Abdallah Seseme, Rashid Ismail, Edward Christopher na Ramadhan
Singano ‘Messi’/Frank Sekule.
Mtibwa
Sugar; Shaaban Hassan Kado, Malikqa Ndeule (16), Yussuf Nguya (5), Salum Swedy
(2), Salvatory Ntebe (20), Babu Ally Seif (17)/Juma Mpakala, Jamal Mnyate (26)/
Hassan Seif (11)/Ally Mohamed ‘Gaucho’, Awadh Juma (27), Hussein Javu (21),
Shaaban Kisiga ‘Malone’ (29) na Vincent Barnabas (13)/Said Mkopi.
0 comments:
Post a Comment