Release No. 201
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 23, 2012
SIMBA YAPATA NAFASI YA TATU KOMBE LA UHAI
Simba
imetwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha
timu zenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada
ya kuitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 3-0.
Hadi
mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 23 mwaka
huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, Simba ilikuwa
mbele kwa bao 1-0.
Mabao
yote ya washindi katika mechi hiyo yalifungwa na Ramadhan Mkipalamoto.
Mfungaji alifunga bao la kwanza dakika ya 43 wakati mengine alipachika
dakika za 57 na 70. Kwa kunyakua nafasi ya tatu, Simba imeondoka na
kitita cha sh. 500,000.
Mechi ya fainali ya michuano hiyo kati ya Azam ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga itachezwa leo (Desemba 23 mwaka huu) saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Mbali
ya kombe, bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said
Salim Bakhresa kupitia maji Uhai atapata sh. milioni 1.5 wakati makamu
bingwa atazawadiwa sh. milioni 1.
Timu
iliyoonesha zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000,
mchezaji bora wa mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na
kipa bora sh. 300,000. Naye kocha bora katika mashindano hayo
atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa bora.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI MUSA RICO
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
mchezaji wa zamani wa timu ya Coastal Union, Musa Rico kilichotokea jana
(Desemba 22 mwaka huu) jijini Tanga.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti
akiwa mchezaji Rico, na baadaye kocha alitoa mchango mkubwa kwa timu
mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Coastal Union, hivyo
mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Rico, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na
uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko
yanatarajiwa kufanyika leo (Desemba 23 mwaka huu) mkoani Tanga. Mungu
aiweke roho ya marehemu Rico mahali pema peponi. Amina
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TAREFA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) uliochaguliwa katika
uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 22 mwaka huu).
Ushindi
waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika
kusimamia mchezo huo mkoani Tabora.
TFF
inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAREFA
chini ya uenyekiti wa Yusuf Kitumbo aliyeshinda kwa kura 16 dhidi ya
nane za Musa Ntimizi, na Paul Werema ambaye hakupata kura.
Uongozi
huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha
shughuli za mpira wa miguu mkoani Tabora kwa kuzingatia katiba ya TAREFA
pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia
tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA na Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi
waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti), Fate
Remtulla (Katibu), Dick Mlimuka (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Razak
Irumba (Mwakilishi wa Klabu TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao
ni Eric Kabepele na Mwalimu Sizya.
TWFA YAWATUZA TENGA, FURAHA FRANCIS
Chama
cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania (TWFA) kimetoa tuzo kwa Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na Meneja wa
timu ya Taifa (Twiga Stars), Furaha Francis kutokana na mchango wao
katika kuendeleza mchezo huo.
Tuzo
hizo zilitolewa katika Mkutano wa Uchaguzi wa TWFA uliofanyika Desemba
19 mwaka huu mjini Morogoro kutokana na mchango wao katika kuendeleza
mpira wa miguu kwa wanawake nchini.
“Ni
dhahiri kazi ya kuendeleza soka ya wanawake ni wajibu wa Shirikisho
(TFF), lakini Rais wa TFF alitoa kipaumbele zaidi na alijitoa
kuhakikisha misingi imara ya kuendeleza soka ya wanawake inawekwa,”
alisema Mwenyekiti wa TWFA, Lina Kessy.
Pia
Mkutano huo ulitambua na kumpa tuzo Furaha Francis ambaye amekuwa
Meneja wa Twiga Stars kwa miaka minane mfululizo. Licha ya kuwa Meneja
wa Twiga Stars, ametumia muda wake na kujitoa katika kuendeleza mpira wa
miguu kwa wanawake.
TWFA itaendelea kutumia michango yao katika mpira wa miguu kwa wanawake nchini.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment