WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema kuwa fedha zote ambazo wenyeviti wa
vitongoji wanaidai Serikali kama posho ya usimamizi wa zoezi la sensa ya
makazi na watu zitalipwa hivi karibuni.
Alitoa kauli hiyo jana jioni
(Jumamosi, Desemba 22, 2012) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya
Kibaoni kwenye uwanja wa shule ya msingi Kakuni ambako pia ni kijijini
kwao akiwa katika siku ya kumi ya ziara yake jimboni kwake Katavi
wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Alikuwa akijibu swali la Bw.
Wejja Hassan mkazi wa kijiji cha Kibaoni ambaye alitaka kujua ni kwa
nini wao wamelipwa posho ya sh. 10,000/- wakati waliacha kazi zao na
familia zao wakati wakizunguka na maofisa wa sensa.
Waziri Mkuu alisema wenyeviti
wote waliofanya kazi kwa siku saba na wale ambao maeneo yao yaliongezwa
siku za ziada watalipwa kwa sababu fedha zimeshapatikana.
“Serikali imeshafanya hesabu
zake na tumebaini jumla ya shilingi bilioni 3.1/- zinahitajika. Fedha
zimeshapatikana na zitalipwa hivi karibuni,” alisema.
Akijibu swali la Bw. Godwin
Mbassa kuhusu kupanda kwa bei ya mahindi kijijini hapo kutokana na wimbi
la viwavi jeshi, Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao kuanza kuweka akiba
ya chakula kwa ajili ya familia zao mara baada ya kuvuna.
“Mnasema bei ya debe moja la
mahindi ni shilingi 15,000/- kwa wenzenu Usevya wanauziwa shilingi
18,000/-. Tatizo la bei halikuja kwa sababu ya viwavijeshi bali ni kwa
sababu ya uzalishaji mdogo msimu uliopita ama kutoweka akiba ya chakula
baada ya kuvuna,” alisema.
“Hili ni onyo kwa wakulima,
inabidi mkishavuna msiuze chakula chote kwa kuzingatia kuwa kuna wakati
bei itapanda. Kwa hiyo jifunzeni kuweka akiba ya chakula ili muuze
zaidi,” alisema.
Alisema kwa wastani kaya moja
inahitaji kuweka magunia 10 -15 kama akiba ya chakula ya mwaka mzima.
“Kwa hiyo mtu akivuna magunia 40 atoe akiba ya familia yake na
yanayobaki auze,” alisema.
Waziri Mkuu alihitimisha ziara
yake jana (Jumamosi, Desemba 22, 2012) kwa kufanya kikao cha majumuisho
ambapo alizungumza na viongozi chama na Serikali wa wilaya za Mlele na
Mpanda katika shule ya sekondari ya Mizengo Pinda iliyoko kata ya
Kibaoni.
0 comments:
Post a Comment