Na Mwandishi wetu,Korea.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Dakta Abdallah Kigoda ametoa rai
kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini Korea kuja kuwekeza katika
sekta mbalimbali za uchumi nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na sekta ya
utalii ambayo amesema ina fursa nyingi za uwekezaji katika Nyanja
mbalimbali kama vile malazi, usafiri na usafirishaji watalii, utalii wa
majini (cruise boat) na kadhalika.
Akizungumzia
zaidi kuhusu utalii, Dk. Kigoda amewaambia wawekezaji hao kuwa
Tanzania ni eneo bora la utalii kwani ni nchi yenye vivutio vizuri na
vya aina yake barani Afrika, hivyo akawahimiza kuja kuitembelea na
kujionea wenyewe kwa macho yao utajiri, uzuri na upekee wa vivutio hivyo
vya utalii ukilinganisha na vile vinavyopatikana katika nchi nyingine
Afrika na duniani kwa ujumla.
Waziri Kigoda
alitumia fursa hiyo kumpongeza mwanamuziki maarufu wa hapa Korea na
mwenye washabiki wengi sana nchini hapa aliyejulikana kwa jina moja la
Choy kwa kazi nzuri ya kuutangaza mlima Kilimanjaro nchini Korea kupitia
sanaa ya muziki “Tanzania ina utajiri wa vivutio vingi vya utalii, kwa
mfano mlima Kilimanjaro uko Tanzania, narudia kwa msisitizo kuwa uko
Tanzania na si nchi nyingine yeyote, na nina mshukuru sana mwanamuziki
Choy kwa kuutangaza mlima huo hapa Korea, alisema waziri Kigoda huku
akishangiliwa kwa makofi.
Waziri
Kigoda ameyasema hayo hivi karibuni jijini Seoul nchini Korea katika
hotuba yake aliyoitoa wakati wa mkutano wa Kibiashara baina ya
wafanyabiashara na wawekezaji wa kikorea takribani 100 kutoka katika
sekta kadhaa chini Korea na ujumbe wa maafisa wa Serikali ya Tanzania
kutoka sekta mbalimbali uliofanyika katika hotel ya Lotte na kuhuduriwa
pia na jumuia ya watanzania wanaoishi nchini Korea.
Alivitaja
baadhi ya vivutio ambavyo Tanzania inajivunia kuwa ni pamoja na mlima
Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika, Bonde la
Ngorongoro ambalo ni maajabu ya nane ya dunia, Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti ambayo ni miongoni mwa maajabu mapya saba ya dunia na Visiwa
vya Zanzibar ambavyo ni maarufu kwa utalii wa fukwe na maeneo ya
Kihistoria.
Pembezoni mwa mkutano huo kulikuwa pia
na maonesho madogo ya utalii wa Tanzania ambapo wawekezaji hao
walipatiwa pia vielelezo kadhaa vya utalii sambamba na maelezo
yaliyokuwa yakitolewa na maafisa kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya hifadhi ya bonde la
ngorongoro (NCAA).
NEW VIDEO:- CHRIS BEE - SIENDI MBALI
7 years ago
0 comments:
Post a Comment