Pages

Home » » WABUNGE MKOA WA IRINGA WAMESHINDWA KUTEKELEZA AHADI ZAO NA ZAIDI WAELEKEZA NGUVU ZAO KWENYE KUPAKANA MATOPE KUPITIA MIKUTANO

WABUNGE MKOA WA IRINGA WAMESHINDWA KUTEKELEZA AHADI ZAO NA ZAIDI WAELEKEZA NGUVU ZAO KWENYE KUPAKANA MATOPE KUPITIA MIKUTANO

WAKATI imepita takriban miezi 21 tangu Uchaguzi Mkuu ufanyike nchini, ahadi nyingi za Wabunge wa mkoa wa Iringa bado hazijatekelezwa majimboni mwao, imefahamika.
Uchunguzi uliofanywa Iringa umeonyesha kwamba, sehemu kubwa ya majimbo sita mkoani humo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali hususan katika masuala ya elimu, maji, afya ya msingi, kilimo, masoko na miundombinu.
Uhaba wa walimu, madawati, chaki, ukosefu wa nyumba za walimu, vitabu vya ziada na kiada ni miongoni mwa changamoto inayoikabili sekta ya elimu mkoani humo, huku kwa sehemu kubwa wabunge hao wakiwa hawajatekeleza ahadi zao walizozitoa wakati wakiomba ridhaa ya wananchi.
Aidha, huduma za maji safi na salama nazo ni duni katika sehemu nyingi, hususan vijijini ambapo wananchi wanahangaika kila kukicha bila msaada wa wabunge wao.
Kwa upande wa kilimo, changamoto kubwa zinazowakabili wananchi ni gharama za pembejeo huku idadi ya vocha za ruzuku ikipungua, ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao mbalimbali kama nyanya, pareto na chai pamoja na mazao mengine.
Imebainika pia kwamba, afya ya msingi ni changamoto kubwa kwa wananchi wengi wa vijijini, ambao wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu katika zahanati na vituo vya afya ambavyo navyo vinakabiliwa na uhaba wa dawa.
Jimbo la Iringa Mjini
Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, katika kutatua kero za wapiga kura wake, lakini imeonekana kwamba bado kuna changamoto nyingi katika maeneo ya jimbo hilo ambazo hazijatatuliwa licha ya ahadi zilizotolewa na Mbunge huyo mwaka 2010.
Changamoto ya miundombinu, hasa ya barabara katika Manispaa na maeneo mengine ya Jimbo hilo ni zimwi linalotishia uhakika wa Mbunge huyo kurejea tena mwaka 2015, huku tatizo la vijana wasio na ajira likionekana kuwa la kudumu.
Hata hivyo, Mch. Msigwa kwa upande mwingine ameweza kutatua kero kadhaa hususan katika sekta ya afya, ambapo Februari 16, mwaka huu wakati alipokabidhi vifaa mbalimbali katika Hospitali mpya ya Manispaa iliyoko maeneo ya Frelimo mjini Iringa.
Vifaa hivyo vilivyokuwa na thamani ya Sh. 50 milioni, ni pamoja na vitanda vya kisasa 30 pamoja na magodoro yake pamoja na baiskeli 19 za walemavu (wheel chairs).
Ilielezwa kwamba, kila kitanda kiligharimu Sh. 1.5 milioni wakati thamani ya baiskeli moja ilikuwa Sh. 700,000 pamoja na vikabati vya kuhifadhiwa vifaa vya wagonjwa katika wodi, fedha ambazo zilipatikana kupitia wahisani wake R.T.C.O.
Wakati akikabidhi vifaa hivyo, Msigwa alisema kamwe hataweza kugawa fedha kwa wananchi, badala yake yuko tayari kusaidia maendeleo kwa hali na mali.
“Nitawasaidia wananchi wote kwa huduma za maendeleo, siyo kuwapa fedha za kula… vitanda nilivyotoa vitawasaidia wananchi wote wa Iringa bila kujali itikadi zao za kisiasa,” alisema.
Jimbo la Isimani
William Lukuvi, ambaye ameliongoza Jimbo la Isimaini kupitia Chama cha Mapinduzi kwa zaidi ya vipindi vitatu sasa, bado anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Hali ya maisha ya wananchi wa Jimbo hilo, ambalo ndilo linaloongoza kwa ukame pamoja na njaa, ni duni mno kwani kilimo, ambacho ndicho pekee wanakitegemea kiuchumi, kimeishindwa kuwainua.
“Mbunge wetu amekuwa akiahidi mambo mengi kila wakati wa uchaguzi, lakini kusema kweli utekelezaji wake hauendani na mahitaji halisi ya wananchi katika kuinua hali yetu ya maisha, pembejeo za kilimo zinachelewa na zinauzwa ghali, tulidhani angetupigania ili wananchi wengi wa hali ya chini tuweze kumudu, lakini wapi,” alikaririwa akisema George Mwanyenza, mkazi wa Nyang’oro.
Inaelezwa kwamba, Lukuvi, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), pamoja na kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri kwa miaka mingi ameishindwa kuinua sekta ya elimu jimboni humo huku shule nyingi zikiwa katika hali mbaya.
Mojawapo ya shule hizo ni ile ya msingi Izazi ambayo hata kiwango cha kitaaluma kiko chini huku uhaba wa madawati ikiwa changamoto kubwa.
Shule hiyo inatumia madawati yaliyotolewa msaada na Paroko mwaka 1986, ambayo yamezeeka na wengi wa wanafunzi wakilazimika kukaa chini.
Uhaba wa nyumba za walimu katika sekondari nyingi za kata jimboni humo ni tatizo jingine ambalo linawafanya walimu wengi wanaopangiwa kufundisha huko washindwe kwenda.
Hata hivyo, kero ya maji jimboni humo, hususan Isimani, inaonekana itapungua kufuatia mkakati wa kuwaunganisha wananchi hao na mradi wa maji wa uhakika ambao umetumia Sh. 5 bilioni utakaovinufaisha vijiji 30 jimboni humo.
Mradi mwingine wa maji, ambao ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Machi, mwaka huu, ni ule wa Pawaga uliojengwa na Kanisa la Anglicana Dayosisi ya Ruaha kwa gharama ya Sh. 2 bilioni.
Mnamo Novemba 25, 2011, Mbunge huyo alikabidhi jumla ya mifuko 1,000 ya saruji yenye thamani ya Sh. 17 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule mbalimbali, mabwawa na nyumba za watumishi jimboni humo.
Jimbo la Kilolo

Jimbo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi hasa upande wa elimu na afya ya msingi, huku ikiwa wilaya inayoongoza kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Kata ya Ilula jimboni humo inakabiliwa na uhaba wa maji ambapo ni asilimia 49 tu ya wakazi wa mji huo mdogo wanaopata maji safi ya bomba.
Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Peter Msolla ameendelea kuikomalia serikali ili ijenge barabara ya kutoka Iringa hadi Kilolo, ikiwa ni miongoni mwa ahadi zake kwa wananchi wa jimbo hilo.
Hata hivyo, Prof. Msolla ni kati ya wabunge ambao kwa asilimia kubwa wamefanikiwa kutekeleza ahadi zao katika sekta mbalimbali.
Mwezi Juni mwaka huu Mbunge huyo alikabidhi kompyuta tatu na vitabu vya kiada, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 9 milioni, msaada uliotolewa na Kampuni ya Simu Airtel Tanzania katika shule za sekondari Mazombe, Maria Consolata na Udzungwa na Mazombe.
Jimbo la Kalenga

Dk. William Mgimwa, ambaye ni Waziri wa Fedha, anakabiliwa na changamoto nyingi katika Jimbo la Kalenga hususan suala la afya, maji na kilimo.
Vijiji kadhaa jimboni humo vinakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa maji pamoja na uhaba wa pembejeo za kilimo hali ambayo inaendelea kudumaza maendeleo ya uchumi jimboni humo.
Jimbo la Mufindi Kaskazini

Mbunge wa Jimbo hilo, Mahmoud Hassan Mgimwa (CCM), naye ana changamoto kubwa jimboni humo kutokana na kutotekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi zake hasa katika sekta ya elimu na afya.
Wakazi wengi wa jimbo hilo wamemtaka arudi jimboni na kutekeleza kwa vitendo ahadi zake, vinginevyo hali itakuwa mbaya mwaka 2015.
Jimbo la Mufindi Kusini

Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM, naye anakabiliwa na changamoto katika suala la kilimo, ambapo wakulima wadogo wa chai wanalalamika kupunjwa na wakulima wakubwa.
Wananchi wa jimbo hilo pia wanalia kutokana na miundombinu mibovu ya barabara ambayo inakwamisha maendeleo.
Aidha, wavunaji wadogo wa miti nao wameendelea kulalamika  kuhusu upendelea unaofanywa na serikali katika ugawaji wa vitalu, jambo ambalo wamesema mbunge huyo anapaswa kulishughulikia kama alivyowaahidi.
Kwa ujumla, wabunge wote wa Iringa, hasa wa kuchaguliwa, wana kazi kubwa ya kutekeleza ahadi zao kwa kuzingatia utawala bora na uwajibikaji.
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Greyson Salufu | Chimbuko Letu Inc | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Mbwile Media - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger