Mkuu wa mkoa wa Mbeya ABASI KANDORO.Picha na Gabriel Mbwille.
|
Na Ester Macha, Mbeya.
Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya Bw.Abbas Kandoro ametoa wito kwa waajiri kutoa nafasi
kwa wafanyakazi kujiendeleza kimasomo katika chuo kikuu huria na vyuo
vinginevyo sanjari na kuwalipia ada na gharama nyinginezo ili kuboresha
mazingira ya kazi,kuleta tija mahali pa kazi pamoja na kuongeza ufanisi
wa utendaji wa kazi.
Wito huo umetolewa na Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya chuo kikuu huria kituo cha Mbeya na kuongeza kuwa chuo kimeanzisha program hizo katika muda muafaka ambapo mfanyakazi anaendelea na kazi huku akipata fursa ya kujiendeleza bila kuathiri shughuli za uzalishaji.
Bw.Kandoro alisema kiwango cha ubora wa elimu kinachotolewa na chuo kikuu huria hakina tofauti na vyuo vingine vya kulala,na kwamba faida nyingine kubwa katika chuo kikuu huria ni gharama zake nafuu hivyo ni fursa pekee kwa wafanyakazi na watanzania wengine kujiunga kwa wingi.
Alisema katika kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho serikali haina budi kupongezwa kwa juhudi zake kwa kuendeleza misingi na fikra za hayati Baba wa taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeanzisha wazo hilo na kuanzia katika vyumba vya kupanga hadi kufikia kuwa na majengo yake ya kujivunia,walimu wenye ubora wa kutosha na rasilimali nyingi.
Hata hivyo Mkuu huyo alioumba uongozi wa chuo kikuu huria kutoondoa kabisa njia ya kufundisha kwa kutumia makaratasi wakati utaratibu mpya ya kusoma kwa kutumia mtandao ukiwa unaendelea ili kutoa fursa kwa wanafunzi waliopo vijijini ambako hakuna umeme wala’ internet’ kuendelea kutumia mfumo huo.
"Lakini muda Fulani msiwalaumu waajiri kutowapatia fursa ya kusoma kwa sababu muda mwingine fedha zinakuwa hakuna na jambo jingine watu wanataka kusoma tofauti na nafasi aliyoajiriwa,na wengi mnakimbilia kusomea utawala,sasa tutakuwa watawala wangapi,"alisema.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliuomba uongozi wa chuo kutumia nafasi ya kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari ili watanzania waweze kupata mwamko na mwitikio wa kujiunga kwa wingi tofauti na ilivyo sasa,"mimi nampongeza Mkurugenzi wa jiji la Mbeya kwa ubunifu amechukuwa matangazo makampuni yanalipia na yamewasha taa, jiji sasa linaendelea kupendeza hata usiku na usalama unakuwepo."
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya , Bw.Juma idd alisema suala la kuwaendeleza wafanyakazi kielimu lipo kisheria hivyo ni jukumu la waajiri kuangalia namna ya kuwapanga wafanyakazi wake bila kuathiri utendaji wa kazi.
Alisema kwa upande wake,Halmashauri ya jiji imewapeleka zaidi ya wafanyakazi 260 masomoni huku wakiendelea na utendaji wa kazi na amewaomba waajiri wenzake waache kuwazuia wafanyazkazi wao wanapohitaji kusoma jambo la msingi ni kuangalia uwepo wa mafungu na nafasi.
Mkurugenzi wa chuo kikuu huria kituo cha Mbeya,Dkt,Michael Ng’umbi alisema kituo kimeshaaza majaribio ya mpango wa mwanafunzi kufanya mtihani muda wowote atakaoona yupo tayari kufanya hivyo na kwamba wanaendelea kuboresha mazingira ya kusomea kwa kuanza kutoa elimu kwa njia ya mtandao ambapo mwanafunzi anajibu maswali na kuyatuma katika kituo kwa njia ya mtandao.
Dkt.Ng’umbi ametaja mikakati mingine ni pamoja na kufungua vituo vidogo katika wilaya ambapo tayari wameshafungua katika wilaya mbili na walimu wa kujitosheleza ikiwemo na kuendelea kuwasiliana na makao makuu ili waweze kupewa bajeti ya kujitangaza katika vyombo vya habari.
Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Bw.Juma Kaponda ameuomba uongozi wa chuo kuangalia kwa makini kuhusu mabadaliko hayo ili yasitoe nafasi kwa baadhi ya wanafunzi kufanyiwa mitihani na watu wengine na hatimaye kupata wahitimu wenye kiwango hafifu na kuangalia udahili ili kupandisha kiwango cha elimu badala ya kushuka.
0 comments:
Post a Comment