Pages

Home » » Mgogoro Wa Ardhi Kapunga - 9

Mgogoro Wa Ardhi Kapunga - 9


Esterina Kilasi, Mbunge wa zamani wa Mbarali ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe
 
Serikali yajichanganya katika
uuzaji wa mashamba ya Nafco
 
HUU ni mfululizo wa Ripoti Maalum kuhusiana na mgogoro wa ardhi Kapunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya kama unavyoendelea kusimuliwa na Mwandishi Wetu DANIEL MBEGA, ambaye aliyefanya uchunguzi kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu kwa ufadhili wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF). Endelea na Sehemu hii ya Tisa…

“Ubepari una nguvu sana. Ni mfumo wa mapambano. Kila bepari anastawi kutokana na kupambana na bepari mwingine.Maneno haya ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yamo kwenye hotuba yake aliyoitoa Januari 2, 1973 mjini Khartoum, Sudan.
Nimeona bora nianze nayo katika makala haya kutokana na ukweli kwamba, tangu Sera ya Ubinafsishaji ilipotamalaki, ikiwa inafuatia lile Azimio la Zanzibar lililouzika Ujamaa na kuusimika ubepari kwa kisingizio cha ‘Uchumi Huria’, ubepari ulitamalaki na mabepari wakaanza kupigana vikumbo kila mmoja akitaka kusimama.
Chambi Chachage na …. Wanaeleza katika ripoti yao ya The state of Nafco farms (Hali ya mashamba ya Nafco), kwamba, uuzaji wa Shamba la Nafco Kapunga ulikwenda sambamba na uuzaji wa Shamba la Mbarali ambalo tangu mwaka 1977 Nafco ilipolichukua kwa Wachina lilitambulika kuwa na ukubwa wa hekta 5,575, lakini lilipouzwa ikaelezwa kwamba lina ukubwa wa hekta 5,842, ikiwa ni ongezeko la hekta 267 ambazo hazijulikani zilikotokea.
Sarakasi za uuzaji wa Shamba la Kapunga, kama ilivyo kwa lile la Mbarali, zilianza wakati Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wakati huo, Charles Keenja, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2003/2004, ambapo alilieleza Bunge kwamba Serikali ilikuwa imeamua kuuza mashamba ya Nafco ya Kapunga, Ruvu na Dakawa, kwa wakulima wadogo.
Hizi zilikuwa habari njema sana kwa wananchi wa maeneo husika, ambao waliamini kuwa sasa wataweza kuzalisha mpunga kwa wingi katika maeneo hayo ambayo tayari yalikwishawekewa miundombinu bora ya umwagiliaji.
Wakati huo, Waziri Keenja alisema serikali ilikuwa inaendelea kufanya tathmini na utaratibu wa namna ya kuyauza mashamba hayo kwa wakulima wadogo ambao ndio watakaoyamiliki.
Lakini katika hatua ya kushangaza, katika kuwasilisha bajeti ya mwaka 2004/2005 kwa wizara yake, Waziri Keenja akasema kwamba, Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC wakati huo) ilikuwa inaandaa utaratibu wa kutangaza kuyauza mashamba ya Kapunga na Mbarali, jambo ambalo hatimaye likafanyika.
Ripoti ya Chachage na mwenzake inaendelea kubainisha kwamba, katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2005/2006, Waziri Keenja alisema mchakato wa kuyauza mashamba hayo ulikuwa katika hatua za mwisho, kwani tayari wakati huo wazabuni walikuwa wamekwishajitokeza.
Kizungumkuti hiki cha miaka mitatu mfululizo, kwa kauli tatu za waziri yule yule kilidhihirisha kwamba, tayari ubepari ulikwishatamalaki na kila bepari alikuwa akiangalia namna gani ya ‘kutawala’.
Itakumbukwa kuwa, katika swali lake la nyongeza kuhusiana na suala hilo wakati wa Kikao cha Bunge Februari 3, 2004, Mbunge wa Mbarali wa wakati huo, Estherina Julio Kilasi, alisema bayana kwamba, mchakato wa kuyauza mashamba hayo ulikuwa umeanza tangu mwaka 2001 na kwamba miaka mitatu ilikuwa imepita bila wananchi kupewa taarifa kuhusu nini kilichokuwa kinaendelea kuhusiana na ama kuuzwa au kugawiwa wao wenyewe.
Naibu Waziri wa Kilimo wa wakati huo, Profesa Pius Mbawala, alijibu tu kwa kifupi kwamba, kwa sababu mashamba hayo hayakuwa ya wananchi kisheria, basi walikuwa ‘wavamizi’. Akasisitiza kwamba, utaratibu wa kuwamilikisha ulikuwa mrefu na kwamba ungetekelezeka ikiwa tu wananchi hao wangefuata taratibu kama alizokuwa amezielezea kwenye majibu yake ya msingi kuhusiana na mashamba ya West Kkilimanjaro.
Chachage na mwenzake wanazidi kubainisha katika ripoti yao kwamba, miaka miwili baadaye, wakati wa Kikao cha Bunge Juni 27, 2006, Mbunge wa Mbarali Esterina Kilasi alirudia tena swali lake kuhusu hatma ya yaliyokuwa mashamba ya Nafco wilayani Mbarali.
Alisema kwamba, mashamba hayo mawili ndiyo yaliyokuwa chanzo pekee cha pato la wananchi wa Mbarali kwani yalihusisha wakazi 30,000 kutoka vijiji 10. Mbunge huyo akasema pia kwamba, mashamba hayo hayakuwahudumia wananchi wa Mbarali tu, bali watu kutoka Iringa na wilaya nyingine za Mkoa wa Mbeya waliokuwa wakilima humo.
Baada ya kubainisha kwamba baadhi ya wawekezaji wameshinda zabuni hiyo ya kuyaendesha mashamba hayo na kwamba kulikuwa na changamoto za mazingira, akaonya kwamba kutoa shamba kwa mtu mmoja au wawili kulikuwa kunawaweka wakulima wengi wilayani humo katika wakati mgumu.
Ili kutafuta suluhu ya mkanganyiko huo, akaishauri serikali kuwahamishia wakulima wadogo waliokuwa pembezoni mwa mashamba hayo na kuwaweka katika sehemu ya mashamba yaliyoendelezwa angalau kwa kuwapatia kila mmoja hekta moja ili kuona kwamba wanalima na kupata mavuno bora ili kujiongezea kipato kwa vile hata vyanzo vya maji pembezoni havikuwa vinakidhi mahitaji ya kilimo.
Kilasi alihoji ni kwa vipi wawekezaji hao hawakupewa maeneo ambayo hayajaendelezwa kwenye Bonde la Usangu wilayani Mbarali kama kweli walikuwa na ujasiri wa kuendeleza kilimo ili mashamba yaliyoendelezwa yabakie kwa wakulima wadogo.
“Kwa hiyo, nimwombe Waziri Mkuu kwamba, wakae tena waangalie kwa sababu hakuna kipato kingine Wilayani Mbarali. Ukizungumza kwamba, kuna chakula safari hii Mbeya, Mbarali uitoe kwa sababu haina mvua, inategemea kilimo cha umwagiliaji na tangu mwaka 1992 baada ya Nafco kushindwa kulima, wakulima wamekuwa wakikodi mle ndani ya mashamba, kwa zaidi ya miaka kumi sasa…Kwa sababu Nafco ilipokuwepo hata wananchi wenyewe walikuwa wanaajiriwa mle ndani, hawakuweza kumudu maisha yao ya kila siku. Lakini baada ya kuambiwa sasa mtakodi yale mashamba na wamekuwa wakilipa Sh 25,000 kwa hekta moja, vipato vimeongezeka.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu ulifika miaka ya 1980, uliona sasa ni tofauti kabisa. Hali ya Mbarali watu walivyoendelea, walivyobadilika, mashule tumejenga kwa kutumia kipato cha kilimo cha mpunga si kitu kingine na kwa mfano tu ulio rahisi, katika hekta moja ya shamba, mkulima akilima pale anapata magunia 40 na akiuza anapata karibu Sh 1.8 milioni, ukitoa gharama inabaki Sh 1.2 milioni kwa hekta moja.
“Sasa kwa mwaka mzima kwa hekta hizo 7,000 ambazo ziko kwenye shamba moja, kuna Sh 8 bilioni ambazo zinazalishwa pale kwenye ile Wilaya na hizo pesa zinabaki ndani ya Wilaya ya Mbarali. Sasa leo akipewa mtu mmoja, sielewi unamfanyaje huyu mwananchi aweze kumudu maisha yake ya kila siku, unampa wapi eneo lingine la kulima akitoka mle ndani ya mashamba?” alipata kusema wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Kilimo.
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Greyson Salufu | Chimbuko Letu Inc | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Mbwile Media - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger