WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameahidi kuchangia gharama za ununuzi wa jenereta kwa ajili ya kata
ya Usevya iliyopo wilayani Mlele mkoani Katavi lakini amewataka
wafanyabiashara maarufu katika kata hiyo wajiunge na kuchangia nusu ya
gharama hizo.
Alitoa ahadi hiyo jana jioni
(Ijumaa, Desemba 21, 2012) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya
Usevya kwenye uwanja wa ofisi ya tarafa akiwa katika siku ya tisa ya
ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
“Nakubali kuwa umeme ni
changamoto kubwa katika kata hii natoa rai kwa wafanyabiashara wa hapa
Usevya, kaeni chini mpange mtachangia kiasi gani ili tupate jenereta
kubwa la kusambaza umeme kwa kaya 300. Tunahitaji sh. milioni 50 ili
kupata jenereta la aina hii,” alisema.
“Kule Majimoto niliwaahidi
kuwachangia nusu ya gharama yaani sh. milioni 25, na nyinyi pia tafuteni
hiyo nusu na mimi nitatoa shilingi milioni 25/-. Lakini, hizo za kwao
zitolewe kama mkopo na hizi za mbunge ziwe msaada. Tukubaliane kuwa
mtarudishiwa umeme ukianza kupatikana ili jenereta liwe mali ya kijiji,”
alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa uliohudhuria mkutano huo.
“Natoa ushauri huu kwa sababu
najua tukiwaachia wafanyabiashara wamiliki hili jenereta na kuuza umeme
wataweka bei kubwa na hii itawafanya watu wengine wakose huduma hii
muhimu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi ameahidi kuwasomesha chuo cha
VETA vijana 16 kutoka katika kata hiyo ili waweze kuendeleza miradi ya
kikundi chao cha ujasiriamali.
“Nimependa ubunifu wa kikundi
cha wajasiriamalai Usevya. Nitamwomba diwani asimamie zoezi hili, tupate
vijana 16 waende VETA wakasimee upishi. Mimi nitawalipia ada na
kuwanunulia vifaa vya kisasa ili waje huku kufanya catering services za nguvu,” alisema.
“Wamesema wakivuna watanunua
mizinga ya kisasa. Mimi nitawapatia mizinga kulingana idadi
watakayonunua. Wakinunua 10 nitawapa 10; wakinunua 20 nitawapa 20;
mkinunua 100 nitawapa 100. Nataka kupitia vijana, watu wengine waone
mabadiliko na waone kuwa jambo la ufugaji nyuki linawezekana,”
alisisitiza.
Waziri Mkuu anahitimisha ziara
yake leo (Jumamosi, Desemba 22, 2012) ambapo atazungumza na wananchi
kwenye uwanja wa shule ya msingi Kakuni kata ya Kibaoni ambako pia ni
kijijini kwao
0 comments:
Post a Comment