JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
ZOEZI LA KUANGAMIZA KUNGURU WEUSI
JIJINI DAR ES SALAAM
Wizara ya Maliasili na Utalii imewataarifu wananchi waishio katika jiji la Dar es Salaam kuchukua tahadhari wakati huu ambapo Wizara inaendesha zoezi la kuwaua kunguru weusi jijini kwa kutumia sumu tulivu iitwayo SRC 1339.
Ingawaje sumu hiyo haina madhara makubwa kwa binadamu, wananchi hasa
watoto, wametakiwa kutocheza na mizoga ya kunguru ambao watakuwa
wamekufa kutokana na sumu hiyo. Endapo mtu atakuwa ameishika mizoga hiyo
anatakiwa anawe kwa sabuni.
Aidha wananchi wametakiwa wasitupe mabaki ya chakula kiholela maana kufanya hivyo ni kukaribisha kunguru katika sehemu husika.
Wizara,
kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali, ilianza kuwaangamiza
kunguru weusi jijini Dar es Salaam tangu mwezi Desemba mwaka 2010 chini
ya mradi maalum unaofadhiliwa na Serikali, kwa kushirikiana na Balozi za
Denmark na Finland, na Shirika la USAID la Marekani.
Tangu
mradi huo uanze mwaka 2010 jumla ya kunguru 750,000 wameshaangamizwa
kwa njia ya mitego maalum na sumu. Hata hivyo ndege hao bado wapo Dar es
Salaam na wanaendelea kuleta kero jijini. Ndiyo maana zoezi la sasa
linafanyika kwa njia ya operesheni ili kunguru wengi zaidi waweze
kuuwawa. Tangu operesheni inayoendelea ianze tarehe 27 Agosti 2012 jumla
ya kunguru 1,000 wameshaangamizwa.
Wananchi
wametakiwa kutoa ushirikiano kwa kikosi kazi ambacho kitahusika kuokota
mizoga hiyo, kwa kuonyesha iliko. Pia wanatakiwa kutoa taarifa pale
watapogundua kuwa kuna idadi kubwa ya ndege hao sehemu yoyote ili hatua
za kuwangamiza ziweze kuchukuliwa.
Taarifa zipelekwe katika ofisi za Manispaa au kwa kupiga simu 0754 498957 (Wilaya ya Kinondoni), 0757 585 358 (Wilaya ya Ilala) na 0714 119200 (Wilaya ya Temeke).
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
1 Septemba 2012
0 comments:
Post a Comment