Pages

Home » » RUSHWA YAANZA KUWAUMIZA WATUNGA SHERIA BUNGENI

RUSHWA YAANZA KUWAUMIZA WATUNGA SHERIA BUNGENI



 BUNGE limeandaa kanuni za maadili ili kuwadhibiti wabunge ambao wanatumia mianya ya kanuni zilizopo kufanya makosa mbalimbali ikiwamo kujihusisha na vitendo vya rushwa. 

Habari zilizopatikana mjini Dodoma na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel zinaeleza kuwa hatua hiyo ya Bunge inatokana na kuongezeka kwa wabunge kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali wanayoyafanya wakiwa nje na ndani ya Bunge. 

Joel alisema masharti hayo mpaka sasa yapo katika hatua ya kuchapwa na kwamba muda siyo mrefu maadili hayo ya kanuni yatatoka. “Tupo katika hatua ya kuichapa code of conduct (Kanuni za maadili) hiyo na kwamba muda si mrefu itatoka na kuanza kutumika.”

 Alisema wamegundua kuwa baadhi ya wabunge wanatumia kanuni za Bunge zilizopo kuzikwepa na kufanya mambo yasiyofaa ambayo yanashusha hadhi ya Bunge, hivyo masharti hayo mapya yatawabana zaidi.

 Kauli hiyo ya Joel inakuja siku mbili baada ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa madai ya kutoa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wazazi uliomalizika jana mjini hapa. Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, alikamatwa na makada wengine wa chama hicho saa 4:30 usiku katika kituo cha mafuta akidaiwa kujaribu kutoa rushwa ya Sh100,000 kwa wajumbe wa mkutano huo wa wazazi. Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari juzi alikaririwa akisema vijana wake walimtia nguvuni Zungu katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake wakiendelea kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa wazazi.

 Mbunge mwingine ambaye ana kesi mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa ni Omar Badwel wa Bahi. Badwel anatuhumiwa kuomba rushwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga mkoani Pwani, Zipora Liana.

 Hatima ya Zungu, Badwel Kuhusu kukamatwa kwa Zungu, Mkurugenzi huyo wa Idara ya Shughuli za Bunge, alisema kuwa Bunge halitamchukulia hatua yoyote na badala yake linaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake. 

Joel alisema suala la Zungu bado ni tuhuma hivyo, ataendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala hadi hapo kama itathibitika kuwa ametenda kosa mahakamani. Alisema suala lake ni sawa na la Mbunge Badwel ambaye ana kesi mahakamani ya kutuhumiwa kujihusisha na rushwa, lakini bado anaendelea kuwa mbunge.

 Hatua hii ya Bunge pia inakuja wakati bado ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma za wabunge kujihusisha na rushwa wakati wa Bunge la Bajeti mwaka huu, ikisubiriwa kusomwa bungeni. Agosti 2, mwaka huu Spika Makinda aliunda kamati ndogo ya kuchunguza tuhuma za rushwa zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya wabunge ambao walidaiwa kwamba walihongwa ili kuikwamisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

 Kuundwa kwa kamati hiyo, kulitanguliwa na tukio la kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Julai 28, mwaka huu pia kutokana na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, kujihusisha na rushwa na wengine kutumia nafasi zao kujinufaisha kwa kufanya biashara na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo lipo chini ya kamati hiyo.

 Mabilioni ya Uswisi Katika hatua nyingine, Serikali imeanza kufanya uchunguzi wa kina ili kujua ukweli na kuwachukulia hatua watu wote walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi. Waziri Mkuu alisema bungeni jana kuwa, mara baada ya uchunguzi huo kukamilika Serikali itatoa taarifa kuhusu uchunguzi huo. Pinda alikuwa akijibu swali aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu jana asubuhi. 

“Jambo hili kwa uzito wake, tumeanza kulifanyia uchunguzi ili kujua ukweli wake na hatua stahiki za kuchukua, tukimaliza tutatoa kauli kama ilivyo kawaida yetu, “ alisema. 

Mbowe katika swali lake alitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kuhusu taarifa za kuwapo kwa mabilioni ya fedha katika akaunti za benki mbalimbali nchini Uswisi ambazo zimewekwa na baadhi ya vigogo serikalini na viongozi wastaafu.

 Katika Bunge la Bajeti lililopita, Kambi ya Upinzani ililiibua suala hilo wakati wa hotuba yao ya Bajeti wakieleza kuwa kuna jumla ya Sh360 bilioni zilizofichwa na baadhi ya Watanzania katika benki mbalimbali nchini Uswisi. 

Taarifa kutoka Benki Kuu ya Uswisi inaonyesha kuwa baadhi ya fedha hizo zimewekwa katika akaunti za vigogo hao na kampuni za mafuta na gesi zilizopo nchini. Jumanne wiki hii, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alipokuwa akichangia azimio la kuridhia marekebisho ya pili ya Mkataba wa Ushirikiano kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP), alisema Serikali iutumie ushirikiano huo kurejeshwa mabilioni yaliyofichwa nchini Uswisi. 

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara Rombo, mkoani Kilimanjaro Oktoba 26 mwaka huu, alimlipua Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk Edward Hoseah, akidai kuwa bosi huyo ameandika barua Uswisi, akieleza kwamba Tanzania haina masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki za nchini hiyo. Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha akisema kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote.

                                              Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Greyson Salufu | Chimbuko Letu Inc | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Mbwile Media - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger