Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akisoma hotuba yake ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa pili wa Wanazuoni
wa Bara la Afrika, ulioanza leo katika Ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar
es Salaam.
Baadhi
ya wageni kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika, waliohudhuria
mkutano huo leo, wakimsikiliza Makamu wa Rais, Dkt. Bilal.
…………………………………………………………………
Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amehimiza umuhimu wa kujenga maelewano mazuri
baina ya wafuasi wa dini mbalimbali, vinginevyo, Bara la Afrika
linaweza kushuhudia migogoro ya kidini kama ilivyoanza kujitokeza huko
Nigeria na hata hapa nchini.
Dk. Bilal ameyasema hayo leo
katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa wanawazuoni wa Bara la Afrika
uliofanyika katika ukumbi wa Karume, PTA viwanja vya Sabasaba, Barabara
ya Kilwa, jijini Dar es salaam.
Alielezea matumaini yake kuwa
mkutano huo utayatafakari matukio mbalimbali ya vurugu za kidini ambazo
zimetokea hapa nchini hivi karibuni kwa lengo la kuweka mustakabali
mzuri wa kuishi kwa kuheshimiana baina ya wafuasi wa dini kuu mbili za
Kiislamu na Kikristo.
“Imani si ugomvi bali imani
inapaswa itujenge kimaadili na moja katika tunu za maadili ni kuishi
vizuri na watu wengine hata kama si wa imani yako,” alibainisha
Makamu wa Rais alisisitiza
umuhimu wa elimu ya mwongozo na ile ya maarifa ya dunia kwa Waislamu na
kusema itawawezesha kutatua matatizo yanayowakabili wananchi yakiwemo ya
uharibifu wa maadili, uasherati, maambukizi ya virusi vya ukimwi,
ukosefu wa ajira na unyanyasaji wa kijinsia.
Alitoa changamoto kwa
wanawazuoni wa Kiislamu na viongozi wengine wa dini kuangalia ni jinsi
gani utandawazi hautoathiri imani na maadili ya waumini lakini pia ni
jinsi gani waumini watanufaika na maendeleo makubwa ya sayansi na
teknolojia yaliyofikiwa na mwanadamu hivi sasa.
Malengo ya umoja huo wa
wanawazuoni Barani Afrika ni pamoja na kutilia nguvu masuala ya elimu,
ushirikiano na kuheshimiana baina ya jamii mbalimbali Barani Afrika.
Makamu wa Rais aliyaelezea
malengo hayo ni mazuri na ya kujenga ambayo kama yakiwekwa katika
matendo, itaondoa ile picha hasi kuwa waislamu ni watu wenye kufarakana,
wasio na elimu, wasioheshimu dini za wengine na wasiotambua nafasi na
mchango wao katika maendeleo ya nchi hizo.
0 comments:
Post a Comment