Pages

Home » » Serikali Kuchukua Hatua Ili Kumiliki Hifadhi Za Madini Ya Makaa Ya Mawe

Serikali Kuchukua Hatua Ili Kumiliki Hifadhi Za Madini Ya Makaa Ya Mawe


 Waziri wa Nishati na Madini akimsikiliza Balozi wa China Bw. Lu Youqing (katikati), kushoto ni Mkalimani aliyeongozana na balozi huyo.

Na:Mohamed Saif

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa serikali inajipanga kuanza kuchukua hatua ili kuiwezesha kumiliki hifadhi yote ya madini ya makaa ya mawe iliyopo nchini kwa kuwa madini hayo ni ya kimkakati.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, madini yote ya kimkakati (strategic minerals), yakiwemo makaa ya mawe yanapaswa kuwa chini ya umiliki wa serikali ili iweze kudhibiti uvunwaji wake na biashara yake kwa ujumla kwa malengo mahsusi yaliyopangwa kwa manufaa ya watanzania.
Akifafanua zaidi, Mheshimiwa Waziri alisema taratibu zote zikikamilika na serikali kutwaa umiliki wa hifadhi ya madini hayo, itaweza kudhibiti matatizo mbalimbali yanayojitokeza katika sekta husika likiwemo la baadhi ya wamiliki wa maeneo yenye madini hayo kuyashikilia kwa muda mrefu wakisubiri kuingia ubia na wawekezaji wengine au kuuza madini hayo nje ya nchi hali inayosababisha watu makini wenye nia ya kuwekeza katika maeneo hayo kushindwa kufanya hivyo kwa kukosa maeneo na hivyo kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.
Waziri alitoa kauli hiyo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na watendaji toka Kampuni ya Sichuan Hongda ya China waliofika kumtembelea wakiongozana na Balozi wa China hapa nchini Mheshimiwa Lu Youqing kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayoigusa sekta ya nishati nchini ikiwemo mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Youqing aliweka bayana kuwa katika mradi huo, kampuni ya Sichuan Hongda inatarajia kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 600 na kwamba megawati 400 kati ya hizo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwaka 2018. Alisema megawati 200 zitatumika kuendeshea mitambo.
Kwa upande wake, Waziri Muhongo aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kufanya mazungumzo na kampuni hiyo ili mradi huo uanze mara moja. Alisema mradi huo umechukua muda mrefu pasipo kuwa na mafanikio na hivyo akasisitiza kuwa umefika wakati sasa watanzania waone mradi huo ukianza kutekelezwa ili wafaidi matunda yake.
Aidha, Profesa Muhongo aliitaka Tanesco kuanza mazungumzo na kampuni hiyo kuhusu ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Mchuchuma hadi Mbeya akifafanua kwamba suala la uzalishaji umeme lazima liende sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji pamoja na usambazaji ili kupata matokeo chanya. 
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Greyson Salufu | Chimbuko Letu Inc | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Mbwile Media - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger