CAF KUKAGUA ‘LESENI ZA KLABU’ JANUARI
Shirikisho la Soka Afrika, CAF, litatuma
Ofisa wake Nchini Mwezi ujao ili kufanya ukaguzi kwenye Klabu za Ligi
Kuu Tanzania kabla ya kutoa Leseni kwa zile ambazo zitakuwa zimekidhi
vigezo vilivyowekwa na hivyo kuruhusiwa kushiriki Mashindano ya CAF.
SOMA TAARIFA ZAIDI:
Release No. 194
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 14, 2012
WAKENYA KUCHEZESHA MECHI YA STARS, ZAMBIA
Mwamuzi Sylvester Kirwa kutoka Kenya
ndiye atakayechezesha mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars
na mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) itakayofanyika Desemba 22
mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kirwa anayetambuliwa na Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) atasaidiwa na Elias Wamalwa na Marwa
Range. Waamuzi hao wasaidizi ambao vilevile watatoka Kenya pia
wanatambuliwa na FIFA.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager tayari iko kambini hoteli ya Tansoma, na
inafanya mazoezi katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na ule wa Uwanja
wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na msisimko wa aina
yake.
MTIBWA SUGAR YAICHAPA TOTO 3-1 KOMBE LA UHAI
Mtibwa Sugar ya Morogoro leo asubuhi
(Desemba 14 mwaka huu) imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Toto
Africans ya Mwanza katika mechi ya michuano ya Kombe la Uhai
inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U20) za
klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.
Juma Luzio alifunga mabao yote matatu
(hat trick) katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume
jijini Dar es Salaam. Alifunga mabao hayo dakika za 44,81 na 88.
Hata hivyo, Toto Africans ndiyo
walioanza kufunga katika mechi hiyo ya kundi A. Bao hilo katika michuano
hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai
lilifungwa dakjika ya 22 na Pastol Makula.
Nayo Simba imenguruma baada ya
kuitandika Mgambo Shooting ya Tanga katika mechi nyingine ya michuano
hiyo iliyochezwa leo asubuhi kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi.
Wafungaji kwa washindi walikuwa Ramadhan Mdoe dakika ya 19, Mohamed
Salum dakika ya 77 na Ramadhan Singano dakika ya 89.
Michuano hiyo inaendelea leo mchana na
jioni. Mechi ya Ruvu Shooting na Kagera Sugar iliyokuwa ichezwe mchana
Uwanja wa Azam, Chamazi sasa itafanyika saa 10 kamili jioni katika
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Mechi nyingine za leo ni Coastal Union
vs JKT Ruvu (mchana- Karume), African Lyon vs Azam (jioni- Chamazi).
Vilevile mechi kati ya JKT Oljoro na Yanga inachezwa leo Uwanja wa
Chamazi.
Kesho (Desemba 15 mwaka huu) ni
mapumziko, na michuano hiyo itaendelea Jumapili kwenye viwanja vyote
viwili- Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na Uwanja wa Azam- Chamazi.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA DRFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linaupongeza uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar
es Salaam (DRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Desemba
12 mwaka huu) hoteli ya Mbezi Garden.
Ushindi aliopata Almasi Kasongo
aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya
Utendaji unaonesha jinsi ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa DRFA walivyo
na imani kwao.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake
kwa Kamati ya Utendaji ya DRFA ambayo hivi sasa ina kinara mpya, na
kwamba ina changamoto kubwa ya kuhakikisha inaendesha shughuli za DRFA
kwa kuzingatia katiba na kanuni.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya
Uchaguzi ya DRFA chini ya Juma Simba na Kamati ya Uchaguzi ya TFF
inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa kuhakikisha uchaguzi huo
unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia katiba na Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF.
Safu mpya ya uongozi wa DRFA inaundwa na
Kasongo (Mwenyekiti), Meba Ramadhan (Makamu Mwenyekiti), Msanifu Kondo
(Katibu), Muhsin Said (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF), Benny Kisaka
(Mwakilishi wa Klabu), Ally Hobe (Mhazini) na wajumbe Mohamed Shabani,
Sunday Mwanahewa na Bakari Mapande.
CAF KUFANYA UKAGUZI WA ‘LESENI ZA KLABU’ JANUARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) litatuma ofisa wake nchini mwezi ujao kwa ajili ya kufanya ukaguzi
kwenye klabu za Ligi Kuu ya Tanzania kabla ya kutoa leseni kwa zile
ambazo zitakuwa zimekidhi vigezo vilivyowekwa. Ili klabu ishiriki
mashindano ya CAF ni lazima iwe na leseni hiyo.
Kwa mujibu wa CAF, ofisa huyo atakuwa
nchini kuanzia Januari 7 mwakani ambapo atafanya ukaguzi huo hadi
Januari 14 mwakani. Mbali ya ukaguzi katika klabu, pia ofisa huyo
atakagua viwanja vitakavyotumika katika mashindano yake na hoteli ambazo
timu kutoka nje zitakuwa zinafikia kabla ya mechi.
Baadhi ya masharti kabla ya klabu kupewa
leseni ya CAF ni pamoja na kuwa na ofisi (physical address), uwanja
wake wa mazoezi, programu ya maendeleo kwa vijana, sekretarieti ya
kuajiriwa, hesabu za fedha zilizokaguliwa (audited accounts) na benchi
la ufundi linaloundwa na watu wenye sifa zinazostahili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment