Ni
baada ya kushindwa kurejesha fedha za CECAFA
L ZFA yafunga milango, haipokei fedha wala msamaha
Na Salum Vuai, Maelezo
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimewafungia kucheza mpira ndani na nje
ya nchi kwa muda wa mwaka mmoja wachezaji sita wa timu ya Taifa Zanzibar
Heroes, kuhusiana na kugawana mgao wa dola elfu kumi walizopata katika
mashindano ya Chalenji hivi karibuni.
Awali, Kamati Tendaji ya chama hicho ilitangaza kuwasimamisha kwa muda
usiojulikana wachezaji wa timu hiyo waliokaidi kurejesha dola mia tano
kila mmoja, walizopata kutokana na mgao huo wa dola elfu kumi walizopata
kwa kushika nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo iliyofanyika Uganda.
Hatua ya kuwafungia wanasoka hao, imekuja kufuatia nahodha wa timu Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ na msaidizi wake Aggrey Morris, kushindwa kufika
ofisi za ZFA Ijumaa iliyopita, walikoitwa kwenda kutoa maelezo kuhusiana
na sakata hilo.
Barua ya ZFA iliyoandikwa Disemba 15, 2012 ikiwa na nambari ya
kumbukumbu ZFA/2/2012 kwenda kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
imewataja wanasoka hao waliofungiwa kwa kile kilichodaiwa utovu wa
nidhamu, kuwa ni, Aggrey Moris, Khamis Mcha, (Azam FC), Nassor Masoud
(Simba SC), Nadir Haroub (Young Africans SC). Twaha Mohamed (Mtibwa
Sugar) na Suleiman Kassim (Coastal Union).
Hata hivyo, katika orodha hiyo yumo pia mchezaji Seif Abdallah
aliyesajiliwa na Azam hivi karibuni akitokea Ruvu Shooting, ambaye ni
miongoni mwa wachezaji waliokuwa wamerejesha fedha hizo awali.
Zanzibar Leo, iliwasiliana na aliyekuwa Meneja Fedha wa Zanzibar Heroes
Said Omar Kwimbi kujua juu ya mchezaji huyo, ambaye alikiri kuwa Seif
alikwisharejesha fedha hizo.
Aidha, uongozi wa ZFA umefahamisha kuwa, baba mdogo wa mlinda mlango
Mwadini Ali ambaye kwa sasa yuko ziarani Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo na klabu yake ya Azam, alifika katika ofisi za chama hicho akiwa
na salamu za familia, kwamba inabeba jukumu la kuzirejesha fedha hizo.
Taarifa ya Kamati Tendaji ya ZFA iliyokutana Novemba 14, mwaka huu
kujadili kitendo cha utovu wa nidhamu kilichofanywa na wachezaji wa timu
hiyo kupora fedha hizo dola elfu kumi kiliamua kuchukua hatua
zifuatazo:
ZFA imewapongeza na kuwasamehe wachezaji wote waliotanabahi na kujutia
kitendo hicho na kuamua kuzirejesha fedha walizochukua.
Aidha pamoja na kukilaani kitendo hicho, ZFA imesema wachezaji wote
ambao wanaendeleza kiburi kwa kukaidi kurejesha fedha hizo wanafukuzwa
mara moja kutoka katika timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), na
hivyo kuzufungiwa kushiriki mashindano yoyote yatakayoandaliwa na ZFA au
kwa kushirikiana na taasisi nyengine kwa muda wa mwaka mmoja.
Aidha, imewazuia kuwemo, kushiriki au kuwa na haki ya kushiriki katika
timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kipindi kama hicho, na kwa
hatua hiyo inawaondoa mara moja katika orodha ya wachezaji wa timu ya
Taifa ya Tanzania.
Taarifa hiyo imesema, kwa kuzingatia kuwa hakuna TFF bila Zanzibar, na
kwamba kuikosea Zanzibar na ZFA ni sawa na kuikosea TFF na Tanzania,
hivyo wachezaji hao wanafungiwa kucheza mpira nje na ndani ya Tanzania
kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Imeelezwa kuwa, utekelezaji wa adhabu hizo unaanza mara moja kuanzia
tarehe ya barua hiyo (Disemba 15, 2012), ambapo TFF imeombwa kutoa
ushirikiano na kuhakikisha kuwa wachezaji wote waliotajwa ambao
wameteuliwa katika Taifa Stars wanaondoshwa mara moja kwenye timu hiyo.
Habari zaidi kutoka ndani ya ZFA zimeeleza kuwa, kufuatia hatua hizo,
kwa sasa hakuna tena nafasi wala mchezaji yeyote aliyekwishafungiwa,
kurejesha fedha hizo, na kwamba hazitapokelewa, wala hakuna msamaha
utakaosikilizwa.
Mbali ya barua hiyo kunakiliwa kwa uongozi wa juu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo na BTMZ, pia nakala zimepelekwa kwa klabu
za Azam, Simba, Yanga, JKT Oljoro, African Lyon na Coastal Union.
NEW VIDEO:- CHRIS BEE - SIENDI MBALI
6 years ago
0 comments:
Post a Comment