JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
Ndugu wananchi,
Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 na 20 Septemba, 2012. Jumla ya wanafunzi 894,881 wamesajiliwa kufanya mtihani huo ambapo wavulana ni 426,285 sawa na asilimia 47.64 na wasichana ni 468,596 sawa na asilimia 52.36. Aidha, kati ya wanafunzi hao, wapo wanafunzi 874,379 watakaofanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 20,502 watafanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo waliyoitumia kujifunzia. Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 92 wakiwemo wavulana 53 na wasichana 39. Watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 495, kati yao wavulana ni 238 na wasichana ni 257.
Mtihani huu utafanyika kwa mara ya kwanza kwa kutumia teknolojia mpya ya ‘Optical Mark Reader’ (OMR),
ambapo watahiniwa watatumia fomu maalum za OMR kujibia mtihani na
majibu yao yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta. Masomo yatakayotahiniwa
katika mtihani huo ni Kiswahili, English Language, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Ndugu wananchi,
Maandalizi
yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na
kusambazwa kwa karatasi za mitihani, kusambazwa kwa fomu maalum za
kujibia mtihani na nyaraka zote zinazohusu mtihani huo. Mafunzo maalum
kwa ajili ya matumizi ya fomu za OMR yamefanyika kwa lengo la kuwaandaa
watahiniwa, wasimamizi pamoja na viongozi wa elimu katika ngazi
mbalimbali ili waweze kutumia ipasavyo teknolojia hiyo.
Ndugu wananchi,
Mtihani
wa Kumaliza Elimu ya Msingi ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla
kwa kuwa unahitimisha ngazi ya Elimu ya Msingi na kufungua milango kwa
ajili ya elimu ya sekondari. Hivyo, matokeo ya mtihani huu hutumika
katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na Elimu ya Sekondari. Kwa
kuzingatia umuhimu wa mtihani huo, napenda kutumia fursa hii kutoa wito
kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa taratibu zote za
mitihani zinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa
mazingira yanakuwa salama na tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza
kusababisha udanganyifu.
Napenda
pia kutoa wito kwa wasimamizi wa mitihani kufanya kazi yao ya kusimamia
kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Wapo baadhi ya wasimamizi
ambao wamekuwa wakishiriki katika kuwasaidia watahiniwa kufanya
udanganyifu kwenye mitihani. Napenda kuwaasa tena wasimamizi
kujiepusha na vitendo hivyo vya udanganyifu kwani serikali haitasita
kuchukulia hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kukiuka
taratibu za mitihani.
Kwa
upande wa wanafunzi watakaofanya mtihani mwaka huu, ninaamini kuwa
walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka saba ya Elimu
ya Msingi. Hivyo, ni matarajio yangu kuwa mtaufanya mtihani huo kwa
utulivu na kuzingatia taratibu zote za mitihani ili matokeo ya mtihani
yaoneshe uwezo wenu halisi kulingana na maarifa na ujuzi mliopata katika
Elimu ya Msingi. Serikali inawaasa wanafunzi wote kutojihusisha na
vitendo vyovyote vya udanganyifu katika mtihani kwani watakaobainika
watafutiwa matokeo yao yote ya mtihani.
Ndugu wananchi,
Natoa
wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha kwamba
mtihani huo unafanyika kwa amani na utulivu wa kutosha bila usumbufu
unaoweza kusababishwa na shughuli za kijamii hasa katika maeneo ya
jirani na shule.
Mwisho,
napenda kuwaasa tena wanafunzi, walimu na wananchi wote kwa ujumla
kujiepusha na vitendo vya udanganyifu wa aina yoyote katika Mtihani wa
Kumaliza Elimu ya Msingi. Nawaomba pia raia wema wasisite kutoa taarifa
katika vyombo husika pindi wanapoona au kuhisi mtu au kikundi cha watu
kinajihusisha na udanganyifu wa aina yoyote katika mtihani huo.
Nawatakia watahiniwa wote heri na fanaka katika mtihani utakaofanyika tarehe 19 na 20 Septemba, 2012.
MHESHIMIWA PHILIPO AUGUSTINO MULUGO (MB)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
0 comments:
Post a Comment