Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa kutoka
Umoja wa Mataifa unaoshughulikia Matumzi endelevu ya Nishati kwa wote,
wakati ujumbe huo ulipofika Ofisini kwa Makamu wa rais, Ikulu jijini Dar
es Salaam, leo Oktoba 17, 2012 kwa mazungumzo.
Picha na OMR
TAARIFA KWA VOMBO VYA HABARI
MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA
MUNGANO WA TANZANIA AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA UMOJA WA MATAIFA NA UMOJA
WA ULAYA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM JUMATANO OKTOBA 17, 2012
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na Ujumbe
kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya Ikulu jijini Dar es Salaam na
kufanya nao mazungumzo ambayo mengi yalijikita katika suala la Nishati
Endelevu katika Tanzania.
Ujumbe huo uliwajumuisha; Bw.
Christopher Jones (Mwenyekiti wa Kamisheni ya Maendeleo ya Umoja wa
Ulaya), Bw. Faouzi Bensarsa (Mshauri wa Nishati Umoja wa Ulaya), Bw.
Luis Gomez Echeverri (Mshauri Mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Masuala ya Matumizi Endelevu ya Nishati kwa wote) na Bw Alberic Kacou
(Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania).
Katika mazungumzo hayo; Bw. Jones
alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais namna Umoja wa Ulaya ulivyo na nia
thabiti ya kushirikiana na Tanzania katika kupanga mipango madhubuti
itakayowezesha sekta ya nishati nchini kukua na hivyo taifa kuondokana
na utegemezi wa nishati hasa ya umeme uliopo sasa.
Pia alifafanua kuwa, Umoja huo
umeshafanya mazungumzo na Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania na
hivyo ni matarajio yake kuwa kupitia ushirikiano baina ya Tanzania na
Umoja wa Ulaya, sekta ya Nishati itapata ahueni katika siku zijazo na
hivyo kuongeza uwezo pamoja na idadi ya watumiaji wa nishati hasa ya
umeme kwa Tanzania.
Kwa upande wake Bw. Bensarsa yeye
alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa
Umoja wa Mataifa kuweka agenda ya nishati kuwa moja ya agenda zake kubwa
na akafafanua kuwa kupitia mpango wa ‘Nishati Endelevu kwa Wote’,
Tanzania itaweza kunufaika na fursa zinazotokana na mpango huo na hasa
sasa ambapo bado kuna tatizo la nishati japokuwa katika miaka michache
ijayo Tanzania inategemewa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati
ambayo itatumika hapa na nje ya mipaka ya Tanzania.
Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa
alieleza pia kuwa, Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali na moja
kubwa ni juu ya kuhakikisha kuwa uzalishaji wa nishati unafanyika kwa
kiwango cha juu hali inayoweza kutoa fursa za kukuza uchumi zaidi,
pamoja na kuhakikisha inashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya nishati
katika kuwekeza kwenye sekta hiyo.
Akizungumza na wageni wake, Mheshimiwa
Makamu wa Rais Dkt. Bilal alifafanua kuwa Tanzania imejipanga vema licha
ya kwamba inahitaji ushirikiano kutoka kwa mataifa wahisani, makampuni
na watu binafsi ili kuwekeza katika uzalishaji wa nishati. Pia
akafafanua kuwa, nchi yetu inavyo vyanzo vingi lakini tatizo kubwa lipo
katika upatikanaji mtaji wa kuvitumia vyanzo hivyo hasa kile cha
Geo-Thermal.
Tena Mheshimiwa Makamu wa Rais
aliwahakikishia wageni wake kuwa, Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa
sekta ya nishati inatanuka na kuondokana na utendaji usioridhisha na
kwamba anatarajia kuwepo mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kimfumo
katika shirika la umeme nchini TANESCO , ili lifanye kazi kwa ufanisi na
kuongeza tija kwa watumiaji nishati ya umeme hapa nchini.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
Oktoba 17, 2012
0 comments:
Post a Comment