Na . Ramadhan Ali na Mwanaisha Mohammed-Maelezo
Askari mmoja wa Jeshi la Polisi F.2105
Coplo Said Abdulrahaman wa Kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi ameuliwa
kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi kazini
majira ya saa 6.30 usiku katika eneo la Bububu.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake Ziwani, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa
amesema mauaji hayo yamesababishwa na fujo za wafuasi wa Jumuiya ya
UAMSHO baada ya kuenea uvumi wa kutekwa Msemaji Mkuu wa Jumuiya hiyo
Sheikh Farid Hadi usiku wa kuamkia jana.
Kamishna Mussa amesema Jeshi la Polisi
linaendelea na msako wa kuwatafuta watu waliofanya mauaji ya Coplo Saidi
Abdulrahaman ili kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani kama sheria za
nchi zinavyowaelekeza.
Amesema mpaka hivi sasa watu 10
wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali yaliyotokana na vurugu za
jana na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa Sheikh Farid
unaendelea.
Ameongeza kuwa kutekwa kwa Sheikh
Farid kunatia mashaka kutokana na mazingira ya kutoweka kwake kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake Said Omar Said ambae alikuwa
dereva wake katika hatua za mwisho maeneo ya Mazizini walipokwenda
kununua umeme.
“Sheikh Farid alimuamuru Said amuache
katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka umeme na wakati huo akaendelea
na mazungumzo na watu wengine walikuwemo ndani ya gari nyengine ndogo
ya NOAH ambayo nambari zake hazijajulikana lakini aliporudi kumchukua
hakumkuta” alisema Kamishana Mussa.
Amesema fujo hizo zilisababisha hasara
kubwa kwa Serikali, Chama tawala na wananchi ikiwemo kuchoma na
kuharibumiundo mbinu ya barabara, kuharibu maskani za CCM za Kisonge na
Muembeladu kwa kuzichoma moto baadhi ya magari kuvunjwa vioo na kuvunja
duka la pombe na kuiba mali iliyokuwemo ndani.
Hata hivyo amedai hali ya Mji wa
Zanzibar kwa sasa ni shwari, wananchi wanaendelea na shughuli zao kama
kawaida na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vyengine vya
ulinzi na usalama vitaendelea kuhakikisha amani inadumu muda wote.
Amewataka wananchi kuendelea kuwa
wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao, na kutoa
taarifa za watu waliohusika na vurugu pamoja na mauaji ya Coplo Said
Abdulrahaman.
Mwisho
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
0 comments:
Post a Comment