TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Watu sita wamekamatwa kwa tuhuma za kumuua Ofisa wa Polisi marehemu Said Abdulrahman.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari kwamba watuhumiwa hao (majina yanahifadhiwa) walikamatwa sehemu tofauti, mmoja amekamatwa Kisiwa kidogo cha Tumbatu, wa pili maeneo ya Mjini Unguja, mtuhumiwa wa tatu alikamatwa ofisi za Idara ya Uhamiaji alikokwenda kushughulikia hati ya kusafiria ili aweze kutoroka hapa nchini.
Kamishna Mussa alisema watuhumiwa wengine watatu wamekamatwa mkoani Tanga ambako walikimbilia kujificha baada ya kufanya mauaji ya Ofisa Polisi Koplo Said Abdulrahman.
“Watu hao walitorokea huko na tunaendelea kuwahoji… tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa uliotuwezesha kufanikisha ukamataji huo,tunavishukuru vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyo katika Shehia mbalimbali kwa kuimarisha ulinzi wa maeneo yao katika kipindi chote cha fujo na vurugu hizo,” alisema Kamishna Mussa.
Kamishna Mussa aliwaambia waandishi wa habari kuwa Polisi hivi sasa inaendelea kuwahoji Sheikh Farid Hadi na viongozi wenzake wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam ili kufahamu wapi alipokuwa na kuthibitisha kama kweli alitekwa ama la.
Katika hatua nyengine Polisi imeonya kuchukua hatua kali dhidi ya wafuasi wa UAMSHO wanaodaiwa kutaka kuvamia kambi za Polisi, kambi za Majeshi na Ofisi za Serikali ya Mapinduzi.
“Natoa onyo kali kwa wananchi wote kuwa hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria, Jeshi la Polisi na Vikosi vyote vya ulinzi na usalama tumejipanga madhubuti kukabiliana na mtu yoyote ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu” alisema Kamishna Mussa.
Akizungumzia hali ya amani, Kamishna Polisi alisema kwamba Mji wa Zanzibar ni shwari kwa sasa na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha ulinzi, tunaomba wananchi wasiwe na hofu na waendelee kutii sheria za nchi bila kushurutishwa, waendelee kudumisha amani katika maeneo yao na pia waendelee kutupatia taarifa za mara kwa mara za hali ilivyo huko wanakoishi.”
Imetolewa na: Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzibar 20/10/2012
0 comments:
Post a Comment