TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
KLABU ya soka ya Simba
inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwenu siku ya leo.
1. Kuhusu Boban
na Nyoso
Wachezaji wawili wa Simba,
Haruna Moshi Shaaban (Boban) na Juma Said Halfan (Nyoso), wamesimamishwa
kuitumikia timu ya wakubwa (senior) kwa sababu na nyakati tofauti.
Moshi amesimamishwa kuichezea
timu ya wakubwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na kutokuwa na heshima
kwa mwajiri (timu). Klabu imempa Haruna muda wa siku 21 kutoa maelezo kuhusu
makosa yake na iwapo atashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha, klabu inaweza
kumchukulia hatua zaidi.
Katika kipindi hicho (siku 21
kuanzia jana), Boban atapokea nusu ya mshahara wake wa kila mwezi na hatapata
marupurupu yoyote yanayohusiana na timu ya wakubwa.
Kwa upande wa Nyoso, uongozi
umemwagiza afanye mazoezi na kikosi cha timu ya pili (Simba B) hadi hapo
atakapoimarisha kiwango chake cha uchezaji.
Hatua hii imetokana na ripoti
ya benchi la ufundi iliyoonyesha kwamba mchezaji huyo amekuwa akifanya makosa
mengi ya kiuchezaji yanayoigharimu na ingawa amekuwa akipewa maelekezo na
walimu, bado amekuwa akirudia makosa yaleyale.
Kutokana na hilo, Nyoso atafanya mazoezi na wachezaji wa
kikosi cha pili hadi walimu watakaporidhika kwamba amejirekebisha na yuko
tayari kutumikia kikosi cha wakubwa.
Katika muda wake wote huo
akifanya mazoezi na timu B, Nyoso atakuwa akipata mshahara wake wa kila mwezi kama kawaida na pia atapata marupurupu wanayopata
wachezaji wa Simba B.
Emmanuel Okwi
Klabu ya Simba inaeleza
kusikitishwa kwake na taarifa za vyombo vya habari vyenye lengo la kuuza
magazeti pasipo kujali athari za habari zenyewe.
Kwa mfano, habari ya kwenye
gazeti la CHAMPIONI la leo ina
kichwa cha habari KATIBU MKUU AMFUKUZA OKWI SIMBA. Hata hivyo, kilichoandikwa
ndani ya habari yenyewe kinamnukuu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu kwenye miaka ya
nyuma.
Gazeti hilo linafahamu kabisa kwamba Simba ina
Katibu Mkuu mmoja tu kwa sasa na anaitwa Evodius Mtawala. Simba haijawahi kuwa
na makatibu wakuu wawili kwa wakati mmoja.
CHAMPIONI linafahamu
ukweli huu lakini kwa sababu inazozijua lenyewe, imeamua kuandika habari hiyo
na kuweka kichwa cha habari cha namna hiyo pasipo kujali athari zake kwa
wanachama wa Simba, Katibu Mkuu aliyepo madarakani kwa sasa na weledi wa fani
ya uandishi wa habari
Kilichoandikwa kwenye habari
hiyo ya CHAMPIONI ni maoni binafsi
ya mwanachama wa Simba na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, kila mtu ana uhuru wa kutoa
maoni yake kuhusiana na jambo lolote ali mradi halivunji sheria za nchi.
Simba
SC inarudia wito wake wa kuvitaka vyombo kubaki kwenye misingi ya
kitaaluma na kuacha kuandika habari zilizotiwa chumvi na kuleta mitafuruku
isiyo na sababu yoyote.
Kikosi
Simba inaendelea vizuri na
mazoezi visiwani Zanzibar kujiandaa na mechi
dhidi ya Azam itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi hii.
Hata hivyo, mchezaji Salim
Kinje ameruhusiwa kuondoka kambini Zanzibar
leo kutokana na kupata msiba wa baba yake mkubwa uliotokea Dar jana.
Uongozi, kwa namna ya kipekee
kabisa, unatoa salamu za pole kwa familia ya Kinje kutokana na msiba huu.
Boniface Wambura
Kwa niaba yangu binafsi na
klabu ya Simba, napenda kumpongeza Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Boniface
Wambura, kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa
miongoni mwa wasimamizi wa shirikisho hilo
katika michuano ya Wanawake itakayofanyika nchini Guinea
ya Ikweta (Equatorial Guinea).
Wambura ndiye Mtanzania pekee
aliyeteuliwa na CAF kutumika kwenye michuano hiyo na jambo hilo ni la faraja kwa tasnia ya habari nchini
ambako Wambura ametokea.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba
SC
0 comments:
Post a Comment