Hata hivyo hali hiyo ni tofauti kwa baadhi ya wazazi na walezi walio na jukumu la kutimiza hayo ambao huwageuza watoto kuwa ni miradi kwa kuwafanyisha kazi ngumu na biashara ndogo ndogo huku wengine wakikatisha masomo ya watoto hao na kuwaozesha.
Sikitiko Mateso(16), mkazi wa Mtaa wa Rosuti, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara ni mmoja wa watoto waliotendewa kinyume na sera hiyo ya mtoto, ambapo baba yake mzazi alimlazimisha kuolewa.
Akiwa ndiyo kwanza amehitimu elimu ya msingi mwaka huu wa 2012 katika Shule ya Msingi Mseto, wilayani Geita, mkoani Geita, Sikitiko alisoma kwa msaada wa Shirika la New Light Children Centre Organisation (NELICO), ndoto yake ikiwa kuwa Mwanasheria.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya mjini Geita, Sikitiko alisema kuwa yeye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto tisa wa familia ya mzee Tamaa Mateso mkazi wa mjini Tarime, familia ambayo hutegemea vibarua vya kulima ili kupata mahitaji ya chakula, mavazi na mahitaji mbalimbali ya kifamilia na kwamba lengo kubwa la kuwa mwanasheria ni kujikita katika kupinga ukatili unaowakumba watoto.
Ndoto hiyo ya Sikitiko inatokana na kunusurika kifo, baada ya kufanyiwa ukatili wa kukatwa masikio na baba mkwe wake, baada ya kukataa kuolewa kwa nguvu na kijana wake wakati huo akisoma darasa la tatu Shule ya Msingi Roseti, wilayani Tarime mkoani Mara.
Anasema kuwa baba yake, mzee Tamaa, aliandaa mazingira ya yeye kuolewa baada ya rafiki yake kumpa taarifa kwamba alikuwa anatafuta binti wa kuolewa na kijana wake, mazungumzo aliyodai yalifanyika kwenye klabu ya pombe za kienyeji.
Akisimulia mkasa huo Sikitiko alisema kuwa akiwa na umri wa miaka 13 ambapo alikuwa darasa la tatu katika shule hiyo ya msingi, baba yake alikuwa akinywa pombe za kienyeji klabuni na rafiki yake aliyemtaja kwa jina moja la Kipanga.
‘’Huyo rafiki yake na baba, akamwabia baba yangu kwamba, ana kijana wake anataka kuoa. Baba akamwambia(rafiki yake), kwamba ampatie mahari kwani nyumbani kwake ana binti na ndiyo mimi. Hilo walikubaliana huko klabuni,’’alisema Sikitiko.
Baada ya makubaliano ya wazee hao, Tamaa aliporudi nyumbani alimwambia Sikitiko anayetambulika pia kwa jina la Rozi kwamba aolewe.
‘’Alipofika nyumani aliniita; “Rozi’’, akaniambia; “Mwanangu nataka uolewe.”
Anaongeza kuwa: “Nilikataa ombi la baba, nikamwambia mimi bado mdogo sana, pia ninasoma darasa la tatu hivyo, siwezi kuacha shule na kuolewa. Baba alikasirika sana.’’
Anaeleza kuwa baada ya kukataa ombi la kuolewa, baba yake alimpa amri akitaka aolewe kwa nguvu, huku akimwambia kwamba, atake asitake, ataolewa na huyo kijana mkazi wa Nyamihutwa Tarime, aitwaye Luis Kipanga .
Sikitiko alisema kuwa baba yake alivyozidi kuwa mkali baada ya yeye kukataa ombi lake, Juni 2008 aliamua kutoroka nyumbani kwao na kuanza safari ya kutembea kwa miguu muda wa saa 11 kwenda kwa mjomba wake eneo la Chibumbai, Tarime.
Hata hivyo, anasimulia kuwa wakati akitoroka, baba yake alikuwa tayari ameshapokea mahari ya Sh300,000 kutoka kwa rafiki yake ili yeye (Sikitiko) aache shule na kwenda kuolewa na kijana huyo.
Anabainisha kuwa baada ya mzee Tamaa kupokea mahari hiyo, mzee Kipanga alimbana ili amtoe yeye kwa ajili ya ndoa, kwani kijana wake(Luis), alikuwa ameshajiandaa kwa mapokezi na kuoa.
Hata hivyo, jitihada za Sikitiko kujiokoa na janga hilo kwa kutoroka nyumbani kwao na kwenda kuishi mafichoni kwa mjomba wake, hazikuzaa matunda kutokana na baba yake kumsaka kila wanapoishi ndugu zake hadi alipomkuta kwa mjomba wake.
‘’Nilikaa kwa mjomba mwezi mmoja na baba alivyonipata, mbele ya mjomba alinidanganya kwa kuniambia turudi nyumbani nikaendelee na masomo, kwani ameirudisha ile mahari iliyotolewa na rafiki yake.’’
“Bila kujua kitakachonipata nilikubali na kuongozana naye hadi nyumbani. Lakini baada ya kufika nyumbani, baba aliniambia kuwa ananipeleka moja kwa moja kwa rafiki yake, ili nikaolewe na kijana wake.”
‘’Tulifika nyumbani kwa rafiki yake baba, ilikuwa saa 2:00 usiku. Baada ya kufika, baba aliniacha hapo nyumbani kwa Luis,’’ anaeleza.
Baada ya kuachwa hapo, siku hiyohiyo mkasa ulianza ambapo mzee Kipanga alimwambia Sikitiko kwamba hawezi kuacha kuolewa na kijana wake ambaye alikuwa amejiandaa kuoa baada ya kutoa mahari nyumbani kwao.
“Kama huwezi kuolewa na mwanangu, nakukata masikio yote. Huwezi kukataa kuolewa na Luis, wakati nimetoa mahari nyumbani kwenu. Hilo haliwezekani, lazima uolewe na huyu kijana wangu,’’ alisema Sikitiko akikariri maneno aliyoambiwa na mzee Kipanga.
Anasimulia kwa uchungu kuwa baada ya kauli hiyo Kipanga alimwambia Luis amfunge kamba Sikitiko mikono na miguu kwa pamoja na kamba hiyo ilipitishwa kwenye mti wa mpapai, kisha wakamlaza kifudi fudi kabla ya kutekeleza kauli yake.
Sikitiko anasimulia kuwa ilikuwa ikielekea saa tatu usiku wa asiyoikumbuka ya mwezi Agosti, mwaka 2008, ambapo akiwa amelala kifudifudi chini ya mti wa mpapai huku akipiga mayowe kuomba msaada, Kipanga alimkata masikio yote mawili na kumjeruhi mabega na vidole vya mkono wa kulia kwa kisu chenye incha kali.
Alizidi kusimulia kuwa, baada ya mwanaume huyo kumfanyia ukatili huo, alimfungua kamba, kisha akamfukuza nyumbani kwake na kumtaka atoke akisema kuwa amekipata alichokuwa akitafuta kwa kukataa kuolewa.
‘’Baada ya kunikata masikio aliniambia hayo ndiyo niliyoyataka kwa kutaa kuolewa na kijana wake na kunifukuza akitaka niende kwetu,” alisimulia kwa uchungu Sikitiko akiongeza:
“Wakati huo, damu nyingi ilikuwa ikivuja masikioni, mabegani na vidole nilivyojeruhiwa na nilijaribu kukimbia nikaanguka chini na kupoteza fahamu kutokana na maumivu na kuvuja kwa damu, hadi nilipojikuta niko katika Hospitali ya Wilaya ya Bomani.
Anasimulia kuwa alikaa katika hospitali hiyo kwa muda wa mwezi mmoja akipatiwa matibabu chini ya msaada wa Kituo cha Kivulini cha jijini Mwanza na baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, ambapo alifanyiwa upasuaji.
‘’Nikiwa Bugando, walinifanyia upasuaji wa masikio kwa kutoa kipande cha nyama ya paja kisha wakaibandika masikioni, ikashonwa ili kurejesha hali ya sikio,’’ anaeleza.
Kuhusu kusikia, Sikitiko alisema kuwa anasikia vizuri kama watu wengine wenye masikio na kwamba hana tatizo la kutosikia, kinyume na alivyotarajia awali, huku akitoa shukrani kwa Kituo cha Kivulini na Shirika la NELICO kwa msaada wanaompatia ili kuendelea na masomo yake.
Mkurugenzi wa NELICO, Paulina Alex alisema kuwa walimpokea Sikitiko mwaka 2009 na kumpeleka katika Shule ya Msingi Mseto kuendelea na masomo yake darasa la nne na kwamba maendeleo yake kimasomo ni mazuri, yanayoweza kumsaidia kutimiza ndoto yake kuwa mwanasheria.
‘’Kwa kweli Sikitiko (Rozi) tuko naye tangu tulipompokea, anaishi vizuri na wenzake na maendeleo yake kimasomo ni mazuri. Sisi NELICO, tutamsaidia kumsomesha, pia kumpatia elimu ya kisaikolojia, ambayo imemsaidia kuishi vizuri na wazazi wake wakati anapoenda likizo,’’alisema Alex.
Kuhusu hatua zilizochukulia dhidi ya mhusika wa tukio la kumkata masikio kwa binti huyo, Alex alisema kuwa mtuhumiwa wa kitendo hicho alikamatwa na kufunguliwa kesi ya jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime na kwamba Shirika la Kivulini, ndilo linalohusika kufuatilia mwenendo mzima wa kesi hiyo.
Sikitiko alisema kuwa anatarajia kufaulu katika mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka huu akisisitiza kwamba ndoto yake ni kusoma hadi chuo kikuu.
‘’Napenda masomo yote, darasani nilikuwa nashika nafasi ya kumi mwisho 18 kati ya wanafunzi zaidi ya 100, kwa hiyo ninatarajia kushinda kwenda sekondari, ndoto yangu ni kwenda chuo kikuu niwe mwanasheria, ambaye nitasaidia watoto wanaoonewa na kufanyiwa ukatili,’’alisema Sikitiko.
Majina yaliyotumika katika makala haya ni ya kubuni ili kulinda hadhi ya mtoto pamoja na maadili.
chanzo mwananchi
0 comments:
Post a Comment