MKAZI mmoja Samwel Liungi (37) wa kijiji cha Suluti kilichopo
wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma amekufa papo hapo baada ya kufukiwa na kifusi
wakati anachimba madini aina ya Gamarine kijijini hapo na polisi inawahoji watu
watatu akiwemo mmiliki wa mgodi huo Godwin Sanga (45) mkazi wa kijiji hicho.
Habari zilizopatikana jana mjini
Songea ambazo zimethibitishwa na Kaimu Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Mrakibu Mwandamizi wa Polisi George
Chiposi, zimesema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 30 mwaka huu majira ya saa
7.30 mchana huko katika kijiji cha Suluti kilichopo nje kidogo ya makao makuu
ya Wilaya ya Namtumbo.
Kaimu kamanda Chiposi amebainisha
kuwa inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, huko katika kijiji cha suluti kwenye
eneo la machimbo madogo ya madini aina ya gamarine yaliyopo kijijini hapo
Liungi alifukiwa na kifusi ndani ya shimo alimokuwa anachimba madini hayo na
kufa papo hapo.
Alisema kuwa mgodi huo,
unaomilikiwa na Sanga, ulikuwa na wachimbaji madini watatu ambao aliwataja kuwa
ni Abi Rashid (37), Bakari Hashim (25) na Liungi ambaye kwa sasa ni marehemu na
kwamba chanzo cha kubomoka mgodi huo bado hakijafahamika.
Hata hivyo, kaimu kamanda Chiposi
alieleza kuwa kufuatia kutokea kwa tukio hilo, jeshi la polisi linawashikilia
watu watatu akiwemo mmiliki wa mgodi huo ambao wanaendelea kuhojiwa ili kubaini
chanzo cha tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment