Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya kuchunguza
kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 Prof.
Sifuni Mchome akiwaonyesha waandishi wa habari baadhi hadidu za rejea
zitakazotumika kupata ukweli kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa
kidato cha nne mwaka 2012.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya kuchunguza
kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 Prof.
Sifuni Mchome (katikati)akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam kuhusu kuanza kwa zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka wadau
mbalimbali. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene
(kushoto) na Bi.Tunu Temu mjumbe wa Sekretarieti ya Tume hiyo.
****** ******
Na Aron Msigwa -MAELEZO, Dar es salaam.
Tume ya Taifa iliyoundwa na Mh. Waziri
mkuu Mizengo Pinda kuchunguza kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa
kidato cha nne mwaka 2012 imewaomba watanzania kuipa ushirikiano kwa kutoa
maoni yao ili iweze kukamilisha majukumu iliyopewa kwa muda na ufanisi
mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof.Sifuni Mchome ameeleza
kuwa tume hiyo ilianza kazi mara baada ya kuzinduliwa na Waziri mkuu
tarehe 2 mwezi Machi mwaka huu na kufafanua kuwa jukumu lililopo sasa ni kuanza
kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa watanzania ili kubaini sababu za matokeo
mabaya ya mtihani huo.
Amesema kuwa tume hiyo pamoja na mambo
mengine imepewa jukumu la kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili
kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu
nchini huku mapendekezo hayo yakizingatia kipindi cha muda
mfupi , kati na kipindi cha muda mrefu.
Prof. Sifuni ameeleza kuwa tume hiyo inafanya
kazi kwa kuzingatia hadidu mbalimbali za rejea zikiwemo kubainisha
sababu za matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012, sababu za kushuka kwa kiwango
cha ufaulu, nafasi ya Halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari
katika halmashauri zake.
Rejea nyingine ni
pamoja na pamoja na kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali
ya matokeo hayo pamoja na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua mara moja kwa
wanafunzi 240,903 waliofeli mitihani yao kwa kupata daraja sifuri.
Amefafanua kuwa tume katika kutekeleza majukumu
yake itapitia mitaala na mihutasari ya Elimu ya Msingi na Sekondari,
kutathimini kiwango na mazingira ya ufundishaji na ufunzaji, kuangalia mfumo wa
upimaji na tathmini ya mitihani pia usimamizi na uendeshaji.
Pia pamoja na mambo mengine tume itatathmini
mchango wa jamii na wazazi/ walezi katika maendeleo ya wanafunzi, hali ya
upatikanaji wa chakula cha mchana, upungufu wa majengo ya shule,madarasa,
maabara na maktaba.
Vilelevile tume hiyo itafuatilia mwamko wa
wazazi katika kufuatilia mkazo wa eliimu kwa watoto na suala la mmomonyoko wa
maadili unaotokana na ukuaji wa utandawazi hususan teknolojia ya Habari na Mawasiliano
na kutathmini athari ya mfumo wa ufundishaji wa mikondo miwili iliyopo
katika shule za Zanzibar.
Aidha mwenyekiti wa Tume hiyo amebainisha kuwa
tume itaanza rasmi kukutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kupata maoni
kuanzia tarehe 11 mwezi huu kwa kuanza na mkoa wa Dar es salaam, Zanzbar na
maeneo mengine nchini kwa kukutana na viongozi wa ngazi mbalimbali za Wizara,
Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Shule, Taasisi mbalimbali za kijamii na
wananchi kwa ujumla na pia kuwasilisha maoni kwenye tume kupitia Mwenyekiti wa
Tume, Tume K4-2012, S.L.P 5909 Dar es salaam au kupitia simu 0737206038,
Barua pepe: maoni@tumek4.go.tz
au kwa kutembelea Tovuti ya tume ya www.tumek4.go.tz.
0 comments:
Post a Comment