Ujio wa Nafco na maombi ya ardhi
HUU ni mfululizo wa Ripoti Maalum kuhusiana na mgogoro wa ardhi
Kapunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya kama unavyoendelea kusimuliwa na
Mwandishi Wetu DANIEL MBEGA, ambaye aliyefanya uchunguzi kwa kipindi
kisichopungua miezi mitatu kwa ufadhili mkubwa wa Mfuko wa Vyombo vya
Habari Tanzania (TMF) kupitia Mpango wa Mafunzo Maalum (Fellowship).
Endelea na Sehemu hii ya Pili…
KAULI mbiu za Siasa ni Kilimo; Ukulima wa Kisasa; Kilimo cha Kufa na Kupona; Chakula ni Uhai; na sasa Kilimo Kwanza, zote zimekuwa na madhumuni ya kuendeleza kilimo ambacho kinatajwa kwamba ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.
Serikali ya Tanzania baada ya uhuru
ilitambua umuhimu wa kukiendeleza kilimo, ambacho hata hivyo kilikuwa na
changamoto nyingi kutokana na kutegemea zaidi mvua za masika na vuli,
ambapo zilipokosekana hali ilikuwa mbaya sana kama ilivyotokea katika
ukame wa mwaka 1966.
Hali hiyo ndiyo iliyoifanya Serikali ya
Tanu wakati huo kuja na kauli mbiu mbalimbali ili kukipa kipaumbele
kilimo kwa kutambua kwamba asilimia 83 ya Watanzania wanakitegemea kwa
uchumi pamoja na kuchangia pato la Taifa.
Katika kutimiza malengo ya mkakati wa
maendeleo kupitia utaratibu wa kujitosheleza kwa chakula Serikali ya
Tanzania iliamua kupanua kilimo cha umwagiliaji kuimarisha juhudi za
uzalishaji za wakulima wadogo katika maeneo yaliyotegemea mvua pekee.
Mwaka 1969 Shirika la Taifa la Kilimo na
Chakula (Nafco) likaanzishwa rasmi likiwa na jukumu la kutekeleza na
kusimamia miradi ya kilimo cha mazao yote, ukiondoa miwa. Nafco ikawa na
majukumu ya kusimamia mazao ya chakula kama mahindi, mpunga na
maharage, na mazao ya biashara kama kakao na minazi huku pia ikihusika
na usafirishaji na uhifadhi wa mazao hayo.
Hadi kufikia katikati ya miaka ya 1970
shirika hilo lilikuwa limefanya kazi nzuri kulinganisha na mashirika
mengine yaliyoanzishwa na Serikali kwa majukumu ya kusimamia shughuli
nyingine za uchumi katika sekta ya umma. Tayari lilikuwa limeanzisha
mashamba makubwa ya umwagiliaji huko Mbarali na Ruvu. Katika program
yake ya maendeleo ya mpunga, Nafco iliamua kutumia umwagiliaji kama njia
ya kukabiliana na ukame, hivyo kuwa na kilimo cha uhakika
0 comments:
Post a Comment