WAKATI imepita takriban miezi 21 tangu Uchaguzi Mkuu ufanyike nchini,
ahadi nyingi za Wabunge wa mkoa wa Iringa bado hazijatekelezwa
majimboni mwao, imefahamika.
Uchunguzi uliofanywa Iringa umeonyesha kwamba, sehemu
kubwa ya majimbo sita mkoani humo bado inakabiliwa na changamoto
mbalimbali hususan katika masuala ya elimu, maji, afya ya msingi,
kilimo, masoko na miundombinu.
Uhaba wa walimu, madawati, chaki, ukosefu wa nyumba za walimu, vitabu
vya ziada na kiada ni miongoni mwa changamoto inayoikabili sekta ya
elimu mkoani humo, huku kwa sehemu kubwa wabunge hao wakiwa
hawajatekeleza ahadi zao walizozitoa wakati wakiomba ridhaa ya wananchi.
Aidha, huduma za maji safi na salama nazo ni duni katika sehemu nyingi, hususan vijijini ambapo wananchi wanahangaika kila kukicha bila msaada wa wabunge wao.
Kwa upande wa kilimo, changamoto kubwa zinazowakabili wananchi ni
gharama za pembejeo huku idadi ya vocha za ruzuku ikipungua, ukosefu wa
masoko ya uhakika kwa mazao mbalimbali kama nyanya, pareto na chai
pamoja na mazao mengine.
Imebainika pia kwamba, afya ya msingi ni changamoto kubwa kwa
wananchi wengi wa vijijini, ambao wanatembea umbali mrefu kutafuta
huduma hiyo muhimu katika zahanati na vituo vya afya ambavyo navyo
vinakabiliwa na uhaba wa dawa.
Jimbo la Iringa Mjini
Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, katika kutatua kero za wapiga kura
wake, lakini imeonekana kwamba bado kuna changamoto nyingi katika maeneo
ya jimbo hilo ambazo hazijatatuliwa licha ya ahadi zilizotolewa na
Mbunge huyo mwaka 2010.
Changamoto ya miundombinu, hasa ya barabara katika Manispaa na maeneo
mengine ya Jimbo hilo ni zimwi linalotishia uhakika wa Mbunge huyo
kurejea tena mwaka 2015, huku tatizo la vijana wasio na ajira
likionekana kuwa la kudumu.
Hata hivyo, Mch. Msigwa kwa upande mwingine ameweza kutatua kero
kadhaa hususan katika sekta ya afya, ambapo Februari 16, mwaka huu
wakati alipokabidhi vifaa mbalimbali katika Hospitali mpya ya Manispaa
iliyoko maeneo ya Frelimo mjini Iringa.
Vifaa hivyo vilivyokuwa na thamani ya Sh. 50 milioni, ni pamoja na
vitanda vya kisasa 30 pamoja na magodoro yake pamoja na baiskeli 19 za
walemavu (wheel chairs).
Ilielezwa kwamba, kila kitanda kiligharimu Sh. 1.5 milioni wakati
thamani ya baiskeli moja ilikuwa Sh. 700,000 pamoja na vikabati vya
kuhifadhiwa vifaa vya wagonjwa katika wodi, fedha ambazo zilipatikana
kupitia wahisani wake R.T.C.O.
Wakati akikabidhi vifaa hivyo, Msigwa alisema kamwe hataweza kugawa
fedha kwa wananchi, badala yake yuko tayari kusaidia maendeleo kwa hali
na mali.
“Nitawasaidia wananchi wote kwa huduma za maendeleo, siyo kuwapa
fedha za kula… vitanda nilivyotoa vitawasaidia wananchi wote wa Iringa
bila kujali itikadi zao za kisiasa,” alisema.
Jimbo la Isimani
William Lukuvi, ambaye ameliongoza Jimbo la Isimaini kupitia Chama
cha Mapinduzi kwa zaidi ya vipindi vitatu sasa, bado anakabiliwa na
changamoto kubwa ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Hali ya maisha ya wananchi wa Jimbo hilo, ambalo ndilo linaloongoza
kwa ukame pamoja na njaa, ni duni mno kwani kilimo, ambacho ndicho pekee
wanakitegemea kiuchumi, kimeishindwa kuwainua.
“Mbunge wetu amekuwa akiahidi mambo mengi kila wakati wa uchaguzi,
lakini kusema kweli utekelezaji wake hauendani na mahitaji halisi ya
wananchi katika kuinua hali yetu ya maisha, pembejeo za kilimo
zinachelewa na zinauzwa ghali, tulidhani angetupigania ili wananchi
wengi wa hali ya chini tuweze kumudu, lakini wapi,” alikaririwa akisema
George Mwanyenza, mkazi wa Nyang’oro.
Inaelezwa kwamba, Lukuvi, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Sera, Uratibu na Bunge), pamoja na kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri kwa
miaka mingi ameishindwa kuinua sekta ya elimu jimboni humo huku shule
nyingi zikiwa katika hali mbaya.
Mojawapo ya shule hizo ni ile ya msingi Izazi ambayo hata kiwango cha
kitaaluma kiko chini huku uhaba wa madawati ikiwa changamoto kubwa.
Shule hiyo inatumia madawati yaliyotolewa msaada na Paroko mwaka
1986, ambayo yamezeeka na wengi wa wanafunzi wakilazimika kukaa chini.
Uhaba wa nyumba za walimu katika sekondari nyingi za kata jimboni
humo ni tatizo jingine ambalo linawafanya walimu wengi wanaopangiwa
kufundisha huko washindwe kwenda.
Hata hivyo, kero ya maji jimboni humo, hususan Isimani, inaonekana
itapungua kufuatia mkakati wa kuwaunganisha wananchi hao na mradi wa
maji wa uhakika ambao umetumia Sh. 5 bilioni utakaovinufaisha vijiji 30
jimboni humo.
Mradi mwingine wa maji, ambao ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete
mwezi Machi, mwaka huu, ni ule wa Pawaga uliojengwa na Kanisa la
Anglicana Dayosisi ya Ruaha kwa gharama ya Sh. 2 bilioni.
Mnamo Novemba 25, 2011, Mbunge huyo alikabidhi jumla ya mifuko 1,000
ya saruji yenye thamani ya Sh. 17 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule
mbalimbali, mabwawa na nyumba za watumishi jimboni humo.
Jimbo la Kilolo
Jimbo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi hasa upande wa elimu na
afya ya msingi, huku ikiwa wilaya inayoongoza kwa maambukizi ya ugonjwa
wa Ukimwi.
Kata ya Ilula jimboni humo inakabiliwa na uhaba wa maji ambapo ni
asilimia 49 tu ya wakazi wa mji huo mdogo wanaopata maji safi ya bomba.
Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Peter Msolla ameendelea kuikomalia
serikali ili ijenge barabara ya kutoka Iringa hadi Kilolo, ikiwa ni
miongoni mwa ahadi zake kwa wananchi wa jimbo hilo.
Hata hivyo, Prof. Msolla ni kati ya wabunge ambao kwa asilimia kubwa wamefanikiwa kutekeleza ahadi zao katika sekta mbalimbali.
Mwezi Juni mwaka huu Mbunge huyo alikabidhi kompyuta tatu na vitabu
vya kiada, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 9 milioni, msaada uliotolewa
na Kampuni ya Simu Airtel Tanzania katika shule za sekondari Mazombe,
Maria Consolata na Udzungwa na Mazombe.
Jimbo la Kalenga
Dk. William Mgimwa, ambaye ni Waziri wa Fedha, anakabiliwa na
changamoto nyingi katika Jimbo la Kalenga hususan suala la afya, maji na
kilimo.
Vijiji kadhaa jimboni humo vinakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa
maji pamoja na uhaba wa pembejeo za kilimo hali ambayo inaendelea
kudumaza maendeleo ya uchumi jimboni humo.
Jimbo la Mufindi Kaskazini
Mbunge wa Jimbo hilo, Mahmoud Hassan Mgimwa (CCM), naye ana
changamoto kubwa jimboni humo kutokana na kutotekeleza kwa kiasi kikubwa
ahadi zake hasa katika sekta ya elimu na afya.
Wakazi wengi wa jimbo hilo wamemtaka arudi jimboni na kutekeleza kwa
vitendo ahadi zake, vinginevyo hali itakuwa mbaya mwaka 2015.
Jimbo la Mufindi Kusini
Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM, naye
anakabiliwa na changamoto katika suala la kilimo, ambapo wakulima wadogo
wa chai wanalalamika kupunjwa na wakulima wakubwa.
Wananchi wa jimbo hilo pia wanalia kutokana na miundombinu mibovu ya barabara ambayo inakwamisha maendeleo.
Aidha, wavunaji wadogo wa miti nao wameendelea kulalamika kuhusu
upendelea unaofanywa na serikali katika ugawaji wa vitalu, jambo ambalo
wamesema mbunge huyo anapaswa kulishughulikia kama alivyowaahidi.
Kwa ujumla, wabunge wote wa Iringa, hasa wa kuchaguliwa, wana kazi
kubwa ya kutekeleza ahadi zao kwa kuzingatia utawala bora na
uwajibikaji.
NEW VIDEO:- CHRIS BEE - SIENDI MBALI
6 years ago
0 comments:
Post a Comment