Sophia
Simba, amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT), amekuwa akisemwa wakati mwingine kwa mafumbo kuhusu
masuala ya mahusiano ya kimapenzi aliyopata kuwa nayo. Katika
mahojiano na RAIA MWEMA, mama huyo, miongoni mwa mambo mengine,
aliamua kuwa muwazi juu ya mahusiano hayo na pia masuala kadhaa
yanayohusu UWT.
Raia Mwema: Wasomaji wetu wangependa kukufahamu kwa
sababu mengi yamekuwa yakisemwa na yakinong’onwa hususan kuhusu elimu
yako; labda kwa vile hawaifahamu vizuri. Unaweza kutupa CV yako kwa
kifupi?
Mama Sophia Simba: Asante kwa kunipa nafasi hii
adimu. Nimefurahi kwamba umeweza kufika ofisini kwangu na kuweza
kuongea na mimi. Nashukuru kwamba umeona upo umuhimu wa watu kunijua
mimi Sophia ni nani hasa.
Ni kweli maneno mengi yamekuwa yakisemwa ambayo hayapendezi, lakini
nitafanyaje? Kwa hiyo, kwa kifupi sana ningependa nikufahamishe
labda pengine kwa kupitia wewe watu watanifahamu.
Mimi naitwa Sophia Simba. Ni Sophia Mathew Simba. Nyambi ni jina
langu la nyumbani. Wazaramo wana majina yao ya ukoo, kwa hiyo mimi ni
Nyambi na mdogo wangu alipewa jina lingine. Nilipokuwa mdogo baba
yangu akasema huyu ni Nyambi.
Kwa kifupi sana, mimi ni mtoto wa mfanyabiashara. Baba yangu
alitokea Kisarawe, kijiji kinachoitwa Sungwi. Baba yangu alisoma
Minaki. Alipomaliza Minaki alirudi hapa Dar es salaam. Baba yangu
aliwahi kufanya kazi mpaka ya uvuvi. Aliacha shule kutokana na umbali
kutoka kijijini kwake Sungwi kwenda Minaki.
Watoto waliokuwa wakitoka bara walikuwa wanasoma boarding, lakini
watoto wa Kisarawe wenyewe walikuwa wanatakiwa watembee umbali mrefu.
Kwa hiyo, kutokana na hiyo alifikia mahali haikuwezekana.
Baba yangu mwanzoni alikuwa Mwislamu. Alikuwa anaitwa Omari Simba.
Kutokana na kusoma pale Minaki, aliamua kubadilisha dini. Baba yangu
alibatizwa katika Kanisa la St. Albans – hili la hapa mjini. Na baada
ya hapo baba yangu aliondoka akaenda Morogoro kufanya shughuli za
biashara.
Kule alikutana na mama yangu, mwanamke wa Kiluguru ambaye naye
historia yake alikuwa Sister wa Roman Catholic. Kwa hiyo walikutana na
wakaoana.
Katika maisha yetu yote tumeishi kama Wakristu wa Roman Catholic.
Mpaka leo mimi ni Mroman Catholic ingawaje kila mtu ananipa dini
ambayo anaitaka. Kwa hiyo, mimi ni mmoja wa watoto tisa. Mimi ni wa
pili.
Raia Mwema: Makazi yenu hasa yalikuwa wapi?
Mama Sophia Simba: Makazi yetu yalikuwa Dar es
salaam na Morogoro. Dar es Salaam tuliishi Bungoni, Ilala. Lakini
tukiwa wadogo kabisa baba yangu alijenga nyumba yake ya kwanza kabisa
Morogoro, Kwa Kingu.
Alifanikiwa sana kwa shughuli za baa. Mimi ni mtoto ambaye
nimesomeshwa kwa pesa za pombe. Baba yangu alikuwa na baa inayoitwa
Uzaramo Bar, Morogoro lakini pia alikuwa na baa inayoitwa Simba Bar.
Kwa hiyo, mimi kufungua vizibo vya bia najua.
Nikiwa bado mdogo nilikuwa nauza mishikaki. Siku zote nyumba yetu
ilikuwa upande baa, upande tunaishi sisi. Kwa hiyo, baba yangu
aliendelea na shughuli za baa muda mrefu.
Raia Mwema: Ulianza shule wapi?
Mama Sophia Simba: Mimi nilianza shule Morogoro
katika shule inayoitwa Kilakala, baada ya hapo nikapelekwa shule ya
boarding inayoitwa Ilonga Middle School, Kilosa. Baada ya hapo
nikasoma Forest Hill Secondary School. Sisi ndiyo waanzilishi wake.
Ule mwaka ambao wanafunzi wengi tuliambiwa hatukuchaguliwa
tuliunganishwa darasa la saba na la nane. Kwa hiyo sisi tulimalizia
darasa la nane. Huo ulikuwa mwaka 1965. Shule nyingi (za binafsi)
zilianzishwa mwaka huo. Shule za Kibohehe, Forest Hill, Mzizima na
Kinondoni, zote zilianza wakati huo.
Baada ya pale nikaenda Kibosho Secondary School. Kwa bahati mbaya
baba akafariki, wakati huo nikiwa nafanya kazi NDC. Kabla hajafariki,
baba alitaka sana nifanye shughuli za biashara, niendeleze biashara ya
familia.
Baada ya kumaliza shule nilichaguliwa nikasomee ualimu lakini
sikwenda, na badala yake nikapata kazi NDC. Hapo NDC nilianza kazi
1971 hadi mwaka 1979.
Baada ya hapo nikaingia Lonrho Group of Companies baada ya kuacha
kazi NDC. Kutoka pale nikaanza kazi Metal Engineering Industries
Development Association (MEIDA) ambayo ilianzishwa na Waswedish.
Nikiwa hapo nikaamua kwenda kusoma. Nilianza mafunzo ya Certificate of
law mwaka 1985. Nilipenda sana kusomea sheria.
Mwaka 1987 nilianza kusomea shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, na nikahitimu mwaka 1992 au 1993. Kuna mwaka hapo
katikati chuo kilifungwa kwa sababu ya kuwapo mgomo.
Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu nikarudi kufanya kazi Metal Industries;
kwani wakati nasoma walikuwa wamenipatia likizo isiyokuwa na malipo.
Baada ya kurudi walinipandisha cheo kuwa legal and administrative
officer; kwani kabla ya kwenda chuo kikuu cheo changu kilikuwa
administrative officer tu.
Wakati niko NDC nilikuwa katibu wa tawi la UWT la NDC na Mama Anna
Mkapa alikuwa mwenyekiti wetu, tulifanya mambo mengi mazuri.
Nilipokuwa MEIDA niliomba pia kuwa diwani wa viti maalumu. Kulikuwa
na uchaguzi mwaka 1993 au 1994. Nikawa diwani hadi 1995. Mwaka 1995
wakasema kuna viti maalumu vya ubunge kwa akina mama. Mimi nikagombea
vitu maalumu.
Mwaka huo wa 1995 nilipata invitation ya kwenda Beijing, China
kuhudhuria mkutano wa wanawake duniani. Nikakataa, nikampa mwenzangu
nikamwambia mimi siendi nitabaki hapa kwa ajili ya kampeni za ubunge.
Sikwenda mimi Beijing kwa sababu ya kampeni hiyo. Kwa hiyo mwaka 1995
Nikashinda, na hivyo nikaingia bungeni.
Mwaka 1995 nilifanya mafunzo ya Post Graduate Diploma on Women Law
kwenye Chuo Kikuu cha Zimbabwe na mwaka 2005 nilifanya Masters ya
Community Economic kwenye Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Thesis yangu
ilikuwa Women and Economic Empowerment in Tanzania.
Mwaka 1972 mimi niliolewa. Mume wangu alikuwa ni mwanasheria wa
Chama cha Ukombozi cha Afrika Kusini cha ANC. Siku zile walikuwa
wakiwaita wakimbizi, lakini wenyewe walikuwa wanataka waitwe freedom
fighters.
Mume wangu aliruhusiwa pia kufanya kazi za uanasheria nchini. Kabla
ya kufariki aliwahi kufanya kazi pia benki. Alikuwa anaitwa Clifford
Zex Senge. Wengi walikuwa wanamwita kwa jina la Cliff. Wanasheria
wengi wanamjua.
Kwa hiyo, niliolewa na Cliff na nikazaa naye watoto wawili. Watoto
hao walikwenda Afrika Kusini kwa baba yao lakini sasa wote wamerudi.
Maisha ya Afrika Kusini ni magumu hayako that easy.
Kuna watu wanasema mimi ni kituo cha polisi, wanaume wananikimbia.
Nilisoma kwenye gazeti (eti) wanaume hawanitaki. Lakini I was married.
Raia Mwema: Uliolewa na Msouth Afrika na kwa bahati
mbaya akafariki dunia. Lakini nasikia ulikuwa na mahusiano na
ulionekana mwaka 1995 ukiwa na Kitwana Kondo, Meya wa zamani wa Dar
es Salaam na mbunge wa zamani wa Ilala. Uhusiano wako na yeye ulikuwa
wa aina gani?
Mama Sophia Simba: Sawa, mimi nilikutana na Mzee
Kondo… Kwanza nakubali nilikuwa na mahusiano naye, na nimezaa naye
mtoto wa kiume. Nilikuwa na Mzee Kondo kutoka mwaka 1975. Nilikutana
naye wakati akigombea ubunge; mimi nikiwa kama mpiga debe wake. Kwa
hiyo tulikutana mwaka 1975 na tukaachana mwaka 1983.
Siyo kama tulioana, hapana, alikuwa boyfriend. Yeye siku zote
amekuwa na mke wake. Kwa hiyo, nilizaa naye kweli mtoto mmoja na mpaka
sasa hivi mimi namuheshimu Mzee Kondo. Na baada ya hapo, mwaka 1983,
ameshaoa mara mbili au mara tatu lakini mimi bado namheshimu mpaka
watu hawaelewi mahusiano yangu mimi na yeye yakoje.
Hata tulipokwenda bungeni watu wengine walidhania ni mtu na mkewe,
lakini mimi sijaolewa na Kitwana Kondo. Namheshimu sana, ni baba wa
mtoto wangu.
Raia Mwema: Sasa tuje kwenye nafasi yako ya
uenyekiti wa UWT. Wewe katika miaka yako hii mitano unataka UWT iwe ya
namna gani baada ya kuvaa kofia iliyovaliwa na wanawake wazito huko
nyuma kama Bibi Titi Mohammed, Sophia Kawawa na Anna Abdallah?
Mama Sophia Simba: Asante kwa swali hilo. Kwanza
nishukuru walionitangulia kwamba wamefanya kazi kubwa. Wao ni role
models ambao tulikuwa tukiwatizama na sisi kufanya kazi chini yao.
Nikiri kwamba nimefanya kazi chini ya Mama Sophia. Alipokuwa
mwenyekiti, mimi nilikuwa katibu wa tawi. Mama Abdallah alipokuwa
mwenyekiti wa taifa, mimi nilikuwa mwenyekiti wa UWT tawi la kata ya
Upanga Magharibi. Kwa hiyo, hawa wote wamekuwa viongozi wangu na
nimewaona walivyokuwa wakifanya kazi.
Mimi katika kipindi hiki cha miaka mitano nitaendeleza yale yote
ambayo nimejifunza kutoka kwao, lakini pamoja na hivyo; mambo
yamebadilika. Itabidi na sisi UWT tubadilike.
Ukumbuke kwamba hapo nyuma mimi nilipoinga UWT nilikuwa mfanyakazi.
Sasa hivi baada ya matawi ya kazini ya chama kuvunjwa, kumekuwa na gap
hapo. Wafanyakazi wengi wapo wapo tu. Wanawake wengi hawapo katika
chama, hawapo katika jumuiya, wapowapo tu.
Wapenzi wengi wa CCM wako kama vile wa Simba na Yanga – hawana kadi,
hawana nini. Kwa hiyo, mimi mkakati wangu mmoja mkubwa ni kuhakikisha
nawapata hawa akina mama. Nitawafuata hukohuko waliko katika maeneo
yao kuwahamasisha kuinga UWT.
Hadi sasa tunaendelea vizuri. Tuna kitengo kizima kinachoelezea jinsi
ya ku-capture na kuwahamasisha akina mama na kuwaambia; na wewe pia
unaweza kuwa mwanachama wa UWT, unaweza kuwa mwanachama wa CCM, usikae
tu bure hivi hivi.
Kwa kufanya hivyo, UWT itakwenda na wakati. Tunawahitaji hawa young
generation twende nao tusiwaache nyuma. UWT isiwe jumuiya ya wazee na
watu wazima tu.
UWT iwe ni jumuiya ya wanawake vijana pia, kwa sababu naamini
ukishirikiana na vijana kuna mengi ambayo utaweza kujifunza. Tunaweza
tukaifanya UWT ikawa hatua moja zaidi kutoka hapa tulipo.
UWT tumejipanga kuanzisha tawi la UWT makao makuu. Na lingine ambalo
tumesema tutafanya ni kuifanya UWT isiwe tegemezi kiasi hicho. UWT
ina mali zake nyingi ambazo zimekuwa dormant kwa muda mrefu. Kwa hiyo,
tunataka tuzitumie ili tuweze kwa kiasi fulani tujitegemee.
Hivi sasa watendaji wote UWT wanategemea ruzuku kutoka CCM. Kwa
hiyo, tunakipa mzigo mkubwa sana Chama cha Mapinduzi. Lazima tuangalie
ni jinsi gani tunaweza tukatumia raslimali tulizokuwa nazo, nadhani
tutaipunguzia mzigo CCM.
Kama nilivyosema siku yangu ile ya kwanza, ni lazima twende na
wakati. Nilitumia maneno: ‘UWT iende na dot com.’ Generation ni dot
com, tusirudi nyuma.
Raia Mwema: Lakini baadhi ya watu wanasema kwamba
labda umeanza na gea ngumu kidogo baada ya Katibu Mkuu wako, Husna
Mwilima kuwa amewajibishwa na Baraza Kuu. Huoni kwamba kitendo hicho
cha kumwondoa ni hatua ngumu kwako?
Mama Sophia Simba: Kwanza nikiri kwamba si jambo
zuri kwamba katibu mkuu wangu imebidi Baraza Kuu limwondoe. Mimi
binafsi siyo kitu ambacho nilitarajia, kwa sababu mimi ndiye
niliyemtafuta yeye na jina lake kulipeleka kwenye vikao vya chama
ili lipitishwe.
Kwa hiyo, hiyo imeonyesha kwamba ni udhaifu kwa upande wangu. Nikiri
kwamba sikulifanyia kazi vizuri lile jina. Pengine nilikuwa sikujiandaa
vizuri. Binadamu kufanya makosa ni kawaida, na pale nilikosea.
Hata hivyo, nilijitahidi sana kufanya naye kazi vizuri. Nimekaa naye
kipindi cha mwaka mmoja. Unapopewa madaraka inabidi kwanza ujifunze,
kwa hiyo nilijitahidi sana kuhakikisha kwamba katibu mkuu huyu,
ambaye mimi mwenyewe nilimtafuta, aweze ku-cope na ile ofisi.
Lakini kukawa kuna matatizo ya… Kwanza huwezi kumfananisha huyo na
akina Thecla Mchauru, Kate Kamba, Dk Msimu ambao kiwango cha elimu yao
kidogo ilikuwa zaidi. Hata Halima Mamuya elimu yake iko juu zaidi ya
huyu.
Huyu alibebeshwa mzigo ambao hakustahili, tulifanya makosa.
Tulimbebesha mzito mkubwa wa kiutendaji. Pengine kisiasa kazi nyingine
angeweza kuzifanya, lakini kiutendaji… Kuna kazi za utendaji zina
miiko yake ambayo kiwango cha elimu yake ilikuwa kidogo kina matatizo.
Raia Mwema: Sawa kulikuwa na makosa, lakini wewe ulimpataje pataje hadi akaukwaa ukatibu mkuu wa UWT?
Mama Sophia Simba: Huyu alikuwa mjumbe wa Baraza
Kuu la UWT, ndicho kitu kimoja ambacho kilinifanya nimteue. Nimekuwa
naye kwenye baraza tokea mwaka 2003. Mimi nimemjua Husna wakati
nikigombea ujumbe wa Baraza Kuu. Kwa hiyo, nilipokwenda Arusha yeye
ndiye aliyenisaidia kutafuta kura, siyo campaigner, lakini ndiyo
nilianza kumfahamu. Lakini nikamfahamu pia ndani ya vikao. Kwa hiyo
nilimjua kwa hivyo.
Na kwa bahati mbaya sana, sikujaribu kuomba ushauri kwa mtu yeyote
kutaka kujua habari zake zaidi. Ndiyo maana nasema nakiri makosa.
Hakuna mtu aliyenishawishi kuhusu yeye.
Raia Mwema: Eneo lile la Maria Hostel kulikuwa na
mpango wa kujenga jengo kubwa kuondoa hali ya utegemezi ya UWT ambayo
umekwishaieleza. Je mpango huu bado upo?
Mama Sophia Simba: Mpango wa kuendeleza kiwanja
cha mtaa wa Lindi cha Maria Nyerere Hostel upo. Tumekuta mpaka na
ramani zimeshachorwa, lakini sisi kamati yetu ya utekelezaji tunataka
tujiridhishe, tutumie utaalamu zaidi. Lile jengo tulilolikuta pale
linataka kujengwa lilikuwa haliendani na wakati.
Kwa hiyo, tulichokuwa tukingojea kwanza ni kupata Baraza la
Wadhamini kwa sababu lile baraza la wadhamini lililopita la UWT,
limemaliza muda wake. Sasa limepatikana jipya. Majuzi walikuwa na
kikao chao cha kwanza cha Baraza la Wadhamini. Mwenyekiti wao ni Mzee
Said El Maamry ambaye ni mwanasheria.
Tumelizindua baraza letu na sasa tunachotaka ni kupata hati ya pale
Maria Nyerere. Maria Nyerere ilikuwa trusteeship ya Tanganyika Women,
sasa hivi ni Tanzania Women. Jina limeshabadilishwa, na sasa
tunangojea hati mpya. Tukishapata hati tutaweza kuwekeza pale na
kujenga kitu kizuri.
Raia Mwema: Kitu kizuri namna gani, kwani mnataka kujenga kitu gani?
Mama Sophia Simba: Tunataka tujenge office blocks
na apartments, na sisi wenyewe tutakuwa na floor moja kwa ajili ya
ofisi zetu. Tutakuwa na ukumbi wetu mkubwa wa mikutano, ni vitu kama
hivyo.
Raia Mwema: Sasa hebu tuelezee kuhusu jengo jipya
lile ambalo lilikuwa makao makuu. Nini mnachotarajia kupata kutoka
hapo kwa sababu nalo lilileta minong’ono.
Mama Sophia Simba: Jengo jipya limekwisha,
linangojea kufunguliwa. Lakini kwa kifupi sana niseme kwamba jengo
hilo jipya haliko chini ya management ya UWT. Jengo jipya mkataba
uliosainiwa ulikuwa ni mkataba wa UWT kulipwa certain amout of money
kwa mwaka, hakuna percentage.
Mkataba uliosainiwa haukuwa mzuri. Kwa hiyo, sisi UWT hatuna eneo
lolote. Sisi tutakuwa tunapata kodi ndogo tu. Kiwanja bado ni cha
kwetu, lakini lile jengo wale tumeingia nao mkataba wa miaka 33. Kwa
hiyo they will run that thing kwa muda wa miaka 33. Sisi tutapata pesa
kidogo.
Naona aibu hata kuzisema. Pesa tutakazozipata kwa mwaka hazisaidii
hata kuwalipa mishahara makatibu wetu wote wa jumuiya lakini ndiyo
hivyo tumejifunza kutokana na makosa.
Raia Mwema: Hivi hakuna namna ya kuweza kukutana na waliowekeza mkajadiliana nao kurekebisha huo mkataba?
Mama Sophia Simba: Mkataba uliopo ni binding,
mkataba umeshaingiwa. Hiyo amount ambayo imefikiwa ni ambayo baada ya
kuzungumza nao wakaongeza. Lakini sisi tunasema tumeshajua pale yeye
anakodisha kwa kiasi gani, basi tunataka tumwambie, basi, na sisi
tuongezee kigogo, lakini hiyo ni subject ya mazungumzo ya sisi na yeye.
Raia Mwema: Bunge linalokwisha kwa sasa lina
wanawake wanaowakilisha majimbo 17. Je, mnao mkakati wowote wa kuweza
kuwasaidia wanawake kuwa na ushindani wa kutosha na wanaume kwenye
majimbo?
Mama Sophia Simba: UWT tayari tumeshatengeneza
mkakati wetu wa kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanajitokeza kugombea
kwenye majimbo. Majimbo siyo ya wanaume, majimbo ni yetu sote kwa
hiyo kuna ziara tumeshajipanga. Tutazunguka nchi nzima kuhakikisha
wanawake wanajitokeza kugombea kwenye majimbo.
Tutahakikisha wanakwenda kupiga kura na kuhamasisha wanawake
kuipigia kura CCM. Kwa hiyo tunakwenda kupiga ndege watatu kwa jiwe
moja.
Naamini itakapofika mwaka 2015 wanawake watakaokwenda kwenye majimbo watakuwa wengi zaidi kwa sababu tumeshawawekea ukomo.
Wengine wamekuwa wabunge wa vitu maalumu kwa miaka 15 na wengine
hivi sasa wameshaingia miaka 20, na bado hawajathubutu kugombea kwenye
majimbo. Lakini kwa sasa mkakati tulionao ni kuhakiksiha wanawake
wengi wanajitokeza.
Raia Mwema: Halmashuru Kuu ya CCM imekubaliana na
pendekezo la Baraza Kuu lako juu ya ukomo wa viti maalumu, lakini
baadhi ya wabunge waliopita wa muda mrefu ambao wanadhani mlikuwa nao,
wanadai mumewatosa. Hayo manung’uniko yao wewe unayajibuje?
Mama Sophia Simba: Nafurahi kupata nafasi hii
nijibu hilo. Suala la ukomo wa viti maalumu halikuanza na mimi. Suala
la ukomo wa vitu maalumu tumeanza kulizungumzia mwaka 1998 au 1999.
Lakini kwa sababu sisi wenyewe tuko mle mle kwenye baraza Kuu,
likaminywa.
Likarudi tena 2000 hadi 2005. Likazungumzwa tukiwa Arusha,
likazungumzwa tukiwa Moshi. Watu wanalipooza kwa sababu kila binadamu
tuna kitu kinaitwa choyo, unajifikiria wewe. Kwa hiyo, lile jambo ni
jambo la siku nyingi. Hao wote wanaolalamika wanalijua, wanaiongopea
jamii.
Suala la ukomo halikuletwa na Sophia Simba, suala la ukomo lililetwa
na Baraza Kuu, isipokuwa kwenda kwenye NEC ndiyo limepelekwa safari
hii.
Tatizo ni kwamba siku zile tulikuwa tunalizungumza kwenye Baraza Kuu
lakini halitoki kwenda NEC. Hivi sasa limekwenda kwenye NEC, na kwa
bahati mbaya sana hao wanaolalamika wengine wameshakuwa wabunge miaka
15, wengine miaka 10.
Baraza Kuu lilisema kuwa nafasi za vitu maalumu ambazo ni za
upendeleo, siyo wapendelewe hao hao tu kila siku. Ziliwekwa ili
kumuwezesha mwanamke aweze kupambana na vile vigezo ambavyo tumesema
vinatufanya wanawake tushindwe kuingia kwenye majimbo nao kwa sababu
ya kuwapo mfumo dume.
Tumesema wanawake kwa sababu ya mfumo dume tuna aibu, hatuwezi
kuongea kwenye majukwaa. Kwa sababu ya mfumo dume wanatutukana (eti)
tunaogopa lakini tunasema pia kwamba mwanamke hana pesa za kwenda
kwenye kampeni.
Sasa Baraza Kuu linasema huyu mwanamke au mama baada ya miaka kumi
amekaa bungeni amekwenda kwenye mikutano, ana pesa anashindwa nini?
Aende zake kwenye jimbo.
Hiyo ndiyo concept tuliyozungumza kwamba tayari ile kazi ya
upendeleo imeshafanya kazi. Imeshamtengeneza huyu mwanamke kuwa
mwanasiasa.
Sisi shida yetu tunakata tuwe na wanawake wanasiasa wengi. Sasa hawa
wanakuwa kama selfish, wanaona wao. Kuna mwingine anathubutu anasema
‘he mimi kule kwangu nikitoka mimi, sina jimbo kule. Lakini kama huna
jimbo wewe ukitoka mwanamke mwingine atachukua nafasi yako, kaa
pembeni.
Kwa hiyo mimi wananionea kusema kwamba nimewacha kwenye mataa. Na
hao kwanza waliokaa wanaosema kwamba nimewatosa, mimi UWT
nimechaguliwa na wanawake wa Tanzania yote.
Na nimechaguliwa; hivyo siyo kazi yangu kulipa fadhila.
Nimechaguliwa niwahudumie wanawake wa Tanzania na kwa kufanya hivyo,
kwa kuweka ukomo baada ya miaka kumi tutaona majimbo mangapi wanawake
watachukua.
Watajitokeza tu, sisi wanawake tunapenda sana kusukumwa. Sasa nenda
hapa, sasa nenda pale. Mama Anna Abdallah aliweza mwaka 2005
kutusukuma. Aliniambia Sophia nenda Ilala, wewe fulani nenda pale.
Isitoshe siku hiyo kwenye Baraza Kuu ajenda ya kuwe na ukomo
haikutoka kwenye kamati yangu ya utekelezaji, ilitoka pale pale
barazani.
Hilo ndilo lililotokea kwa hiyo kina mama popote walipo naomba
wasilichukulie hilo kama ni langu binafsi isipokuwa hofu ya wale
wanaotaka waendelee na wasiotaka wenzao wengine wapata hizo nafasi
ndiyo iliyofanya waende wakapeleke hadithi hizo.
Lakini siku moja wataniona shujaa. Kwa suala hili kulipeleka kwenye
NEC ilikuwa kazi kubwa, lakini imewezekana. Hata hivyo, NEC imesema
lisianze mwaka 2010, litaanza mwaka 2015. Mwaka 2015 ni keshokutwa tu
panapo na uhai. Kwa hiyo tutaona sura mpya zinaingia.
0 comments:
Post a Comment