CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimetangaza mkakati wa Uchaguzi Mkuu 2015 kikiahidi kumwaga pikipiki
katika tarafa zote nchini kwa ajili ya kuwafikia wananchi kuelekea
uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo
jana katika kikao cha viongozi wa chama hicho na wadau wake
kilichofanyika hapa.
Mbowe alisema pikipiki hizo zitakuwa na vipaza
sauti maalumu zitawasaidia viongozi wa chama hicho kufanya kazi kwa
ufanisi zaidi.
“Tumeanza mkakati wa kuhakikisha tunawafikia
wananchi kila mahali. Tunataka kusikiliza matatizo yao, na hata pale
ambako kuna shida ya usafiri, kwa pikipiki tutafika,” alisema.
Tayari chama hicho kimezindua kampeni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), ambayo lengo lake ni kuwaandaa wananchi kwa uchaguzi ujao.
Tayari chama hicho kimezindua kampeni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), ambayo lengo lake ni kuwaandaa wananchi kwa uchaguzi ujao.
Mbowe alisema upatikanaji wa pikipiki hizo
unatokana na fedha za ruzuku ambazo zinatolewa na Serikali kwa chama
hicho pia marafiki na wanachama wake walioko nje ya nchi.
Aliwataka viongozi wa chama hicho katika ngazi zote kufanya kazi kwa kujituma ili kuhakikisha kinashika dola mwaka 2015.
“Tanzania inahitaji mabadiliko na sisi tukiwa
viongozi tunapaswa kujipanga kwanza, kuhakikisha tunaongeza wanachama
pia kuzitatua kero za wananchi,” alisema Mbowe.
Katika mkutano huo, Mbowe aliwapongeza viongozi wa
Chadema, Wilaya ya Hanang’ kwa kazi kubwa waliyoifanya kiasi cha kupata
na madiwani 17 katika halmashauri hiyo.
Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Manyara,
Rose Kamili alisema chama hicho kimejipanga kutwaa Jimbo la Hanang’
katika uchaguzi ujao na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.
“Katika miaka hii mitano Chadema, Hanang’ tumekuwa
na mafanikio makubwa na hili linatokana na mshikamano mkubwa wa
viongozi katika ngazi mbalimbali,” alisema.
0 comments:
Post a Comment