Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akiendelea
kuvutia maongezi mazito hata baada ya kutoa hotuba
Dokta Hamza na wenzake katika chai baada ya semina
David Luhanga (kushoto) na Rajab Juma wamezama ndani ya
mjadala wa katiba na usafiri.
Sista Lucia wa kanisa la Wakatoliki aliyeshaishi Tanzania
akiuliza maswali kuhusu ajali ya meli Zanzibar wakati wa mkutano huo wa Central
Hall, Westminster.
Mtayarishaji wa mkutano, Andrew Coulson -ambaye
ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Birmingham- akipiga gumzo kwa chai na mmoja wa
wahudhuriaji.
Waziri Mwakyembe akihutubia semina
Dk Mwakyembe akisikiliza hoja mbalimbali kwa makini
kutoka kwa wananchi ughaibuni wanaolilia
shida za usafiri Bongo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara Tanzania London, Yusufu
Kashangwa, akibadilishana mawazo na Waziri, huku wadau wakisikiliza kwa uchu
Mjadala uliomzunguka Waziri
Aseri Katanga, anayeendesha kituo cha kusafirisha
tarakilishi (kompyuta) kwa wanafunzi wa Bongo toka Uingereza akiwa mjadalani na
Billy Mwangamilo na George Kantande.
Picha zote na
Freddy Macha
Habari na Picha za Freddy Macha
Waziri
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewahakikishia Watanzania na wageni
kwamba jitihada zitaendelea kufanywa na serikali kuboresha usafiri
Bongo.
Akiongea mjini London juzi katika “mkutano wa mwaka” wa jumuiya ya
Watanzania na Waingereza (Britain-Tanzania Society) na Mfuko wa Udhamini
wa Maendeleo (Tanzania Development Trust), alisema bado pana mengi
sana ya kufanya toka ateuliwe miezi minne iliyopita.
Waziri
Mwakyembe vile vile alifafanua kuhusu majadiliano ya katiba mpya
inayotegemewa kutajwa mwaka 2015.
Akijibu maswali toka kwa Wazungu na Watanzania waliohudhuria kikao
Central Hall, Westminster, hatua chache karibu na Ikulu ya Uingereza
(Whitehall), Mwakyembe ambaye ni mbunge wa Kyela, alifahamisha kuwa moja
ya tatizo lililojaribu kutafutiwa ufumbuzi karibuni ni kuzorota kwa
bandari ya Dar es Salaam.
Alisema
Wizara ilibidi kubadili uongozi wa bandari hiyo baada ya ripoti ya
kimataifa iliyoichamba Dar kuwa moja ya bandari mbaya duniani
zisizotekeleza kazi zake sawasawa.
“Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kulisha uchumi wa nchi nzima
ikiendeshwa vyema,” aliueleza mkutano uliomsikiliza kwa makini.
“Tumezungukwa
na nchi nyingi zisizo na bahari ambazo zinatutegemea kusafirisha mizigo
yake. Kwa hiyo basi, wizara ya uchukuzi ikilala na taifa zima
linalala.”
Akitoa mifano kadhaa ya hali mbaya ya usafiri nchini, Dk Mwakyembe
aliongelea kwa hamasa na matumaini kuhusu ujenzi wa barabara na reli
mbalimbali.
“Tuna
mengi bado ya kufanya. Reli zetu kubwa ni za kale sana. Ya toka Dar hadi
Kigoma na Mwanza mathalan ilijengwa enzi za Wajerumani kwa hiyo yabidi
kutengenezwa upya.”
Alitoa
mfano wa ufumbuzi wa tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es
Salaam ambapo pesa zilizopangwa kurekebisha njia nyingine mikoani
zimetumika kurahisisha usafiri kati ya Ubungo hadi mjini na Makanga
hadi Kurasini ( kwa nauli nafuu ya shilingi 500) na muda mfupi wa dakika
ishirini.
Akiwaelemisha waliokuwepo kuhusu maendeleo ya kisiasa Tanzania, Waziri
alisema mjadala unaosisimka nchini sasa hivi unahusu mageuzi ya katiba
ambayo “inatakiwa ioane na maisha ya karne ya 21.”
Akifafanua historia ya katiba Tanzania kwa lugha fasaha ya Kiingereza,
Waziri huyu ambaye ni mtaalamu wa sheria, alitaja miaka muhimu kuwa
1961( baada ya Uhuru),1963 (Ujenzi wa taifa jipya), 1965 (Muungano),
1977 ( kuzaliwa CCM) kisha 1983 na kupitishwa sera ya vyama vingi mwaka
1992.
Maswali mengi yaliulizwa kuhusu usafiri na ulaji rushwa uliochangia sana
uzorotaji unaoendelea kusababisha ajali kubwa na za kutisha bara na
visiwani.
Na
hata baaada ya hotuba rasmi, wakati wa kupata chai, wananchi na wageni
waliendelea kumsonga na kumzunguka Waziri wakimjuza kwa maswali moto
moto. Kiongozi hakuonyesha dalili zozote za kuchoshwa na shauku hiyo.
Akimshukuru
Waziri, mmoja wa maofisa wa Jumuiya ya Waingereza na Watanzania, Bi.
Valerie Leach (anayeendesha shughuli za kielimu Bongo) alisema inawapa
wageni moyo kwamba Tanzania inao viongozi wanaokinzana na rushwa na
ufisadi kama ilivyokuwa enzi zile za Mwalimu Nyerere.
Mapema Dk Harrison Mwakyembe alikaribishwa kwa maelezo ya namna
alivyoshaokoka kufa mara mbili (ajali ya gari na maradhi ya ngozi)
kutokana na msimamo wake kujaribu kuendeleza jamii.
Mapema mkutano ulielezwa miradi mbalimbali inayoendelezwa na Mfuko wa
Udhamini wa Maendeleo (Tanzania Development Trust).
Kati
ya miradi hiyo ni kukarabatiwa nyumba ya wazee Tanga, uendelezaji wa
viwanda vidogo vidogo 37 bara na visiwani, maendeleo ya vijana
wasiokuwa na kazi na vifaa vya wafanyakazi wa hospitali ya Lindi kuepuka
kipindupindu.
Akielezea mapenzi yake kusaidia maendeleo Tanzania, mwanamakati wa
Jumuiya ya BTS, Julian Marcus alisema jitihada za wanachama zinatokana
na michango binafsi na kujitolea bila malipo yeyote.
Shughuli hii ya Jumamosi vile vile ilihudhuhuriwa na Balozi wetu
Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe na Mkurugenzi wa kituo cha biashara
London, Yusufu Kashangwa.
Jumuiya ya BTS ilianzishwa mwaka 1975 na Waingereza na Watanzania
kuendeleza mahusiano kati ya nchi hizi mbili. Inaongozwa na Rais wa
zamani, Ali Hassan Mwinyi.
Kikao
kijacho cha BTS kitafanyika chuo kikuu cha lugha za Kiafrika na Asia
(School of Oriental and African Studies-SOAS) London kujadili demokrasia
na vyombo vya habari Tanzania, tarehe 6 Desemba.
0 comments:
Post a Comment