-Alitakiwa kutumikia adhabu ya mumewe
aliyetuhumiwa kumuua mwanakijiji mwenzo.
-Polisi wamuokoa yeye na mumewe na kuwaficha
kusiko julikana.
Na Moses Ng’wat,Mbeya.
MWANAMKE mmoja, ShidaHasanya, amenusurika
kuzikwa akiwa hai, akitakiwa kutumikia adhabu ya mumewe aliyetoroka baada ya
kutuhumiwa kuhusika kumuua mwanakijiji mwenzake kwa imani za kishirikina.
Tukio hili ni la pili kutokea mkoani
hapa, ambapo Aprili 28 mwaka huu, wananchi wa kitongoji cha Itezi Magharibi,
katika kata ya Itezi, Jijini Mbeya, waliamua kumzika akiwa hai mkazi mwenzao
Nyerere Kombwee, wakimtuhumu kumuua mtoto wa mdogo wake kwa imani za
Taarifa za tukio hilo ziliibuliwa juzi na
Diwani wa viti maalumu, Veronika Mzumbwe (CCM), wakati akitoa ushahidi wa kisa
mkasa katika maadhimisho ya kongamano la kutafakari siku 16 za ukatili wa
kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP) na yanatarajia kuhitimishwa leo.
Akitolea ufafanuzi zaidi diwani huyo, alisema
kuwa tukio hilo ambalo lilimtokea mwanamke huyo baada ya mumewe kutoroka,
lilitokea Disemba 5 mwaka huu, katika kitongoji cha Ihenga, kata ya Isuto
wilayani Mbeya Vijijini.
Alisema maamuzi hayo ya wanakijiji yalifikiwa
baada ya mume wa mwanamke huyo, Shila Njela, ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji
hicho, kudaiwa kutoroka baada ya kutuhumiwa kuhusika na kifo cha mwanamke mmoja
kijijini hapo aliyetajwa kwa jina la Sala Maisha (Mama Hawa) .
Inadaiwa kuwa marehemu Mama Hawa alikufa katika
mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuibuka ugomvi kati yake na
Mwenyekiti wa kijiji hicho, ugomvi unaosadikiwa kusababishwa na biashara ya
Samaki.
Ilielezwa kuwa siku chache kabla ya mwanamke
huyo kufariki, inadaiwa kuwa Mwenyekiti huyo alifika nyumbani kwa marehemu na
kununua Samaki, lakini katika hali ambayo haikueleweka aliwarudisha Samaki hao,
ndipo marehemu aligoma kuwapokea na kuibuka ugomvi.
Inadaiwa kuwa baada ya kurushiana maneno
makali, siku chache baadae marehemu huyo aliyekuwa mfanyabiashara wa
samaki alianza kuumwa na kupelekwa Mjini Mbeya kwa ajili ya matibabu na baadae
kufari, jambo walilomtuhumu Mwenyekiti wao kuhusika na kuamua kutaka kumzika
akiwa hai badala ya marehemu.
“Wakati familia ya marehemu ikiandaa mipango ya
mazishi ya ndugu yao , ikiwemo kuchimba kaburi, kulianza kuibuka tetesi
msibani hapo kuwa kundi la vijana lilikuwa limepanga kulipiza kisasi kwa
kutaka kumzika kiongozi akiwa hai kwa imani kuwa yeye ndiye aliyehusika na kifo
hicho” alifafanua diwani huyo.
Aliongeza kuwa baada ya Mwenyekiti huyo kupata
tetesi hizo ghafla aliamua kutoroka eneo hilo la msiba ambako alikuwa
anaendelea na ukusanyaji wa fedha za michango ya msiba.
Mzumbwe alisema baada ya vijana hao kubaini
kuwa mwenyekiti huyo katorokea kusiko julikana waliamsha hasira na kwenda
kumfuata mke wake nyumbani, ambapo walimfanyia vurugu .
“Mwanamke yule hakuwa na namna, kwani
walipombana wakiwa wamemzunguka alikiri kuhusika na vitendo vya ushirikina kwa
kushirikiana na mumewe na baadhi ya watu kijijini hapo”.
Alisema baada ya maelezo hayo vijana hao
walimtaka alipe kiasi cha shilingi 720,000 kama gharama za usumbufu kwa wao
kuchimba kaburi la sivyo wangezika akiwa hai badala ya mumewe aliyefanya
kitendo hicho na kukimbia.
“Tunashukuru kwani wakati yote hayo
yakiendelea kumbe kuna baadhi ya viongozi wa Kata hawakupendezwa na mpango huo
waliamua kutoa taarifa polisi ambao walifika majira ya saa kumi wakiwa na
silaha hivyo kundi hilo la vijana lilisambaratika kwa kukimbilia kusiko
julikana” alisema Mzumbwe.
Aliongeza kuwa polisi kwa kushirikiana na
polisi walitumia Diplomasi kuwarudisha vijana hao kwa ahadi ya kutokamatwa mtu
yeyote na walikubali na kuzika marehemu majira ya saa tatu usiku.
Alisema baada ya kumaliza kusaimamia maziko
hayo walimchukua mwanamke huyo aliyenusurika pamoja na mumewe ambaye alikuwa
amehifadhiwa na wasamaria wema na kuondoka nao, ambapo hadi sasa hawajarudi
kijijini hapo.
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Diwani Athman,
amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi baada ya kufanikiwa
kuwaokoa watu hao wamewahifadhi kwa mmoja wa ndugu, wakati wakisubiri taratuibu
nyingine zaidi juu ya tukio hilo .
“Ninachoweza kusema ni kweli tukio hilo
limetokea, kazi ya jeshi la polisi ni kulinda usalama wa kila raia, watu hao
tuliwaokoa na kuwatoa huko na sasa tunawahifadhi mahali Fulani kwa ndugu
yao…..kwani si vizuri kupataja maana huwezi juwa wale watu bado wanafikiria
nini juu yao na jumatatu (yaani leo) tutaenda kukutana na wananchi hao kwa
ajili ya kutoa elimu zaidi” alisema Diwani.
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza kwa njia ya
simu na Mwenyekiti huyo ambaye hivi sasa anaishi uhamishoni kusikojulikana na
kukili kukumbwa na mkasa huo, huku akiomba apewe nafasi zaidi ya kupumzika bada
ya kulieleza jambo hilo kwenye vyombo vya habari.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment