Mahmoud Ahmad,Arusha
…………………………..
JESHI la polisi mkoani Arusha
linamshikilia na kumhoji mwanasheria maarufu jijini hapa,Deogratias
Urasa kwa tuhuma za kufyatua risasi hovyo katika ugomvi baina yake na
mfanyabiashara maarufu,James Ndika anayeishi jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa jana na kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoani
Arusha,Liberatus Sabas alisema kwamba tukio hilo lilitokea mwishoni mwa
wiki iliyopita katika mgahawa maarufu wa ViaVia uliopo mkabala na ofisi
ya mkuu wa mkoa wa Arusha.
Mgahawa wa Viavia umejijengea
umaarufu kwa kutembelewa na raia wa wageni kutoka nchi za Ulaya,Marekani
na Asia ambapo katika siku za hivi karibuni umekumbwa na matukio ya
watu kupigana hovyo.
Kamanda,Sabas alisema kwamba
pamoja na mwanasheria huyo anayefanya kazi kutoka kampuni ya Maro
Advocates ya jijini Arusha kufyatua risasi tatu hovyo hewani lakini
katika tukio hilo hakuna mtu yoyote aliyejeruhiwa.
Alitaja chanzo cha ugomvi katika
tukio hilo ni baada ya kutokea majibishano makali baina ya mwanasheria
huyo na Ndika yaliyosababishwa na masuala ya kibiashara miongoni mwao.
“Hawa watu wana mambo yao ya
kibiashara sasa siku ya tukio walijibishana ndipo huyu mwanasheria
akachukua silaha yake na kufyatua risasi hewani hovyo hali iliyopelekea
kuleta taharuki”alisema Sabas
Alisema kwamba mara baada ya
majibishano hayo mwansheria huyo alikosa uvumilivu na kufyatua risasi
hewani hali iliyopelekea taharuki ndani ya mgahawa huo na kupelekea
watu kukimbia hovyo huku wengine wakilala chini kuhofia usalama wa
maisha yao.
Kamanda,Sabas aliliambia gazeti
hili kwamba baada ya jeshi lake kupokea taarifa lilimshikilia
mwanasheria huyo katika kituo kikuu cha polisi cha kati na kisha
kumwachia huru ambapo kwa sasa yuko nje kwa dhamana.
Alienda mbali na kusisitiza ya
kwamba mbali na kushikiliwa jeshi lake lilimhoji mwanasheria huyo juzi
atika makao makuu ya jeshi hilo mkoani hapa na pindi uchunguzi
utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu makosa yanayomkabili.
Alisisitiza kwamba mbali na
kushikiliwa kwa mwanasheria huyo pia jeshi lake linawasaka watuhumiwa
wawili(majina yao yamehifadhiwa) wanaotajwa kuhusika kwa ukaribu katika
tukio hilo .
0 comments:
Post a Comment