Maafisa wa uchaguzi nchini Ghana wamesema vituo 225 vya kupigia kura vimefunguliwa tena leo ili zoezi la kupiga kura liendelee kwa siku ya pili baada ya hapo jana uchaguzi hzuo kuchelewa kuanza kutokana na sababu za kiufundi.
Msemaji wa Tume ya Uchaguzi ya Ghana, Christian Owusu-Parry amesema chini ya asilimia moja ya idadi jumla ya vituo vya kupigia kura vimefunguliwa tena leo. Jana vituo vingi vya kupigia kura vilikumbwa na matatizo ya mashine za umeme za kusomea alama za vidole. Matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa Jumanne ijayo, ingawa katika baadhi ya majimbo tayari matokeo yameanza kutolewa.
Uchaguzi huu unatarajiwa kuwa uchaguzi wa sita wa amani kwenye nchi hiyo ya Afrika Magharibi yenye idadi ya watu milioni 25. Ghana inaonekana kama nchi ya mfano yenye kuzingatia demokrasia barani Afrika. Katika uchaguzi huo, Rais wa sasa John Dramani Mahama kutoka chama tawala anapambana na mpinzani wake Nana Akufo-Addo.
0 comments:
Post a Comment