Na Mwandishi wetu
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi amesema wanawake
wanaweza kuwa viongozi wazuri na mfano wa kuigwa katika maeneo
mbalimbali endapo watajengewa mazingira na kuandaliwa mapema tangu
wawapo shuleni.
Bi. Liundi ambaye pia ni Mkuu wa
Idara ya Habari na Mawasiliano ya TGNP ametoa changamoto hiyo leo katika
Shule ya Sekondari ya Loyola ya jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni
rasmi katika maadhimisho ya siku ya mwanamke shuleni hapo.
Akizungumza na umati wa wanafunzi
wasichana wa shule hiyo na wageni anuai waalikwa, alisema tafiti nyingi
zilizofanywa zinaonesha kuwa wasichana wanapoandaliwa mazingira mazuri
ya elimu wanafanya vizuri ukilinganisha na wavulana.
Aidha aliongeza kuwa kwa sasa
zipo shule zinazochukua wasichana pekee ambazo zimekuwa zikifanya vizuri
zaidi jambo ambalo linaonesha wazi mazingira mazuri yakijengwa jamii
hii inaweza kuinuka na kuwa mfano mzuri.
Alisema kwa sasa vishawishi na
changamoto anuai zilizopo katika shule nyingi ndio kikwazo kwa wanafunzi
wa kike kufanya vizuri, hali ambayo ikifanyiwa kazi kiufasaha
mabadiliko kimafanikio kwa kundi hilo yanaweza kutokea.
Hata hivyo alisema tafsiri
iliyojengeka ya kwamba wanafunzi wa kike wanaogopa masomo ya sayansi si
sahihi kiuhalisia, kwani mazingira ambayo wanafunzi hawa wanakumbana
nayo ndio kikwanzo katika mafanikio yao kimasomo.
“Mfano shule nyingi za kata ni za kutwa wanafunzi hasa wasichana wanakaa mbali
na shule, wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi
shuleni…wanakumbana na changamoto nyingi njiani hivyo wanajikuta
wanashindwa kufanya vizuri au kukatishwa kabisa masomo yao,” alisema Bi.
Liundi.
0 comments:
Post a Comment