Wavunaji wadogo wakimsikiliza Waziri Kagasheki.
Waziri Kagasheki akizungumza na wavunaji wadogo wa Sao hii.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA
MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
Utangulizi
Waziri wa
Maliasili na Utalii Mhe Khamis Kagasheki amesema kuwa Wizara yake inathamini sana
mchango mkubwa unaotolewa na wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka
Shamba la Miti Sao Hill na kuwa Wizara itahakikisha kuwa wananchi hao wanaendelea
kufaidi matunda yanayotokana na shamba hilo ili waendelee kushiriki katika
kulitunza.
Waziri Kagasheki
alisema pia kuwa sheria na busara sharti itumike katika kutatua migogoro ya
uvamizi katika shamba la miti Saohill.
Mheshimiwa
Kagasheki aliyasema hayo katika nyakati tofauti alipotembelea Wilaya ya Mufindi
Mkoani Iringa juzi Ijumaa na jana Jumamosi tarehe 26 Januari 2013 kwa nia ya kusikiliza
kero zilizopo wilayani humo kuhusiana na Shamba la miti la Saohill. Akiwa huko alifanya
mikutano na uongozi wa Mkoa wa Iringa, uongozi
wa Wilaya ya Mufindi, watumishi wa Shamba la miti Saohill Madiwani wa Wilaya
Mufindi na Wavunaji wa Wadogo wa Miti katika shamba la Saohill.
Katika mikutano
yote alijulishwa kuwa kuna kero mbili kubwa zinazolihusisha shamba la miti
Saohill. Kwanza ni mgawo wa miti ya kupasua mbao kutoka katika shamba hilo
ambao ulielezwa kuwa kwa mwaka 2012/13 haukuridhisha.
Pili ni kero ya wananchi
kukosa ardhi ya kulima na kupanda miti kwa kuwa wameongezeka, hivyo wamevamia
sehemu ya Shamba la Saohill na kulima mazao ya chakula pamoja na kupanda miti
yao.
Kamati ya Mgawo
Akizungumza na
watumishi wa Shamba la Miti Saohill Waziri Kagasheki alisema kuwa baada ya
kusoma na kuitafakari taarifa ya ugawaji atawachukulia hatua waliohusika na mgawo
wa mwaka 2012/13 hususan, Meneja wa Shamba aliyekuwepo wakati wa mgawo huo na Msaidizi wake, pamoja na mameneja wa tarafa
za shamba la Saohill. Hatua hizo zitakuwa pamoja na kuwasimamisha kazi ili
wapishe uchunguzi kuhusu mgawo ulivyofanyika. Kwa sasa mamemeja hao
wamehamishiwa vituo vingine.
Vibali vya Uvunaji
Katika mkutano wa
Waziri Kagasheki na wavunaji wadogo, wavunaji hao walimwambia Waziri kuwa utaratibu
wa uvunaji kwa mwaka 2012/13 ulikuwa
mbovu kwa kuwa kulikuwa na kigezo cha kuwa na mashine ya kuchana mbao kwanza
ndipo mwombaji afikiriwe kupewa malighafi.
Wavunaji walisema
kuwa , ili kukidhi kigezo hicho, walinunua mashine, wengine kwa mkopo, lakini
baadhi yao hawakupewa mgawo. Walilalamika pia kuwa baadhi ya wale waliopata
mgawo waliamua kuuza mgawo wao kwa wenye mashine maana wao hawakuwa nazo.
Hata hivyo, katika katika kikao hicho, wadau wengine, kama
vile chama cha kupasua mbao cha SAFIA, walisema
wanaridhika na utaratibu mpya wa mgawo uliowekwa na Wakala wa Huduna za Misitu
(TFS) ambao nia yake ni kukomesha biashara ya ulanguzi katika biashara ya mbao.
Kuhusu ugawaji
wa miti ya kupasua mbao kwa wadau, Waziri Kagasheki alikubaliana na malalamiko
ya wavunaji wadogo, kuwa utaratibu uliotumika katika kugawa miti mwaka 2012/13 haukuwa
mzuri na usingeweza kutenda haki maana wajumbe wa Kamati ya Ugawaji ni Meneja
na wasaidizi wake. Alisema haiwezekani watu wanaohusika na kuuendeleza na
kuutunza msitu huo kutenda haki wakati wa kugawa mazao.
Waziri Kagasheki
aliahidi kuwa ataiunda upya Kamati ya mgawo wa miti ya kuvuna katika Shamba la
Saohill. Aidha Waziri Kagasheki alisema kuwa atavifuta vibali ambavyo havikutolewa
kihalali ili vigawiwe upya.
Uvamizi
Waziri Kagasheki
alipata fursa ya kutembelea Kijiji cha Kibengu kujionea hali ya uvamizi wa
misitu ulivyo. Katika kijiji hicho baadhi ya watu katika kitongoji cha Mgwao walivamia
msitu wakajenga makazi na sasa wameshi ndani
ya hifadhi kwa muda wa miaka 30.
Waziri Kagasheki
alisema kuwa mwaka jana kamati mbili ziliundwa, moja ya Wizara na nyingine ya
Kitaifa, ili kuchunguza migogoro ya mipaka ya hifadhi nchini. Taarifa za kamati
hizo ambazo zilifika Saohill sasa zinachunguzwa ili mapendekezo yake yachangie
katika kutoa uamuzi kuhusu uvamizi katika Shamba la Saohill na sehemu zingine
za hifadhi nchini.
Awali, akisoma
taarifa ya Wilaya ya Mufindi kwa Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Evarista Kalalu
alisema kuwa wanachi wa vijiji sita vikiwemo Ihomasa na Udumuka vimevamia eneo la misitu ya asili
iliyoko Sao Hill, kama vile Mufindi Scarp, na kufanya shughuli za kilimo kwa
kati ya miaka 10 hadi 40.
Vile vile, Mkuu
wa Wilaya ya Mufindi alisema kuwa eneo la zaidi ya Hekta 1,000 linalomilikiwa
na Samba la miti Saohill limevamiwa na watu
wanaotokea vijiji vya Wamimbwale, Usokami, Kibengu, Igeleke, Mapanda na
Kitasengwa vyote vya Wilaya ya Mufindi kwa muda wa kati ya miaka 25 hadi 30.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Simu: +255 784 468047
0 comments:
Post a Comment