SHILINGI bilioni mbili zilizokuwa zimetengwa katika bajeti
ya halmashauri ya wilaya ya Kyela, kwa ajili ya ujenzi wa stendi mpya ya
kisasa, hazikupelekwa ndani ya halmashauri hiyo.
Imeelezwa kutokana na hali hiyo, halmashauri hiyo iliweza
kutumia sh.milioni 100, zilizotokana na vyanzo vyake vya ndani, kuanza ujenzi
wa stendi hiyo katika awamu ya kwanza.
Kipija ambaye ni diwani wa kata ya Kyela mjini, aliyasema
hayo wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya miaka 36 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), yaliyofanyika katika viwanja vya Siasa, Kyela mjini.
Mwenyekiti huyo aliongeza katika bajeti ya mwaka huu, pia
wametenga kiasi kingine cha shilingi milioni 100, kwa ajili ya kuendelea na
ujenzi wa stendi kuu hiyo ya mabasi yaendayo wilayani.
Aliwataka wafanyabiashara wanaomiliki vibanda vilivyojengwa
kiholela katika maeneo yanayoizunguka stendi hiyo, waanze mara moja kuyabomoa
ili kupisha ujenzi wa stendi mpya.
“Kuna vibanda zaidi ya 50 ambavyo vinatakiwa kubomolewa, ili
kupisha ujenzi wa stendi awamu ya pili, hivyo ni vyema kwa wamiliki hawa
kuvibomoa wenyewe vibanda vyao ama sivyo halmashauri itavibomoa vyote” alisema
Kipija.
Katika hatua nyingine, Kipija alikemea tabia baadhi ya viongozi
wa vyama siasa, kikiwemo CHADEMA kuwashawishi wafanyabiashara wanaonunua mazao wilayani
kutolipa ushuru.
Alisema hilo
ni kosa, kwani kwa kuwajali wafanyabiashara hao, halmashauri hiyo iliwapunguzia
ushuru huo kutoka asilimia 5 hadi kufikia asilimia 2.5, lakini bado wanasiasa
wamekuwa wakiwashawishi kutolipa.
Alisema wakulima wa wilaya hiyo, ndiyo ambao hawatakiwi
kulipia ushuru wa mazao yao,
bali wafanyabiashara wanaoenda kununua mazao hayo kwa ajili ya kwenda kuyauza
wilaya nyingine ni lazima walipie ushuru.
“Ni vyema watendaji wa vijiji kwa wilaya nzima wazingatie
hili, wafanyabiashara wa mazao wanatakiwa kulipia ushuru wa asilimia 2.5 na
hili hatutaki kuja kusikia halitekelezwi” alisema Kipija.
Mwenyekiti wa halmashauri alisema wanaendelea na ujenzi wa
daraja litakalounganisha kata ya Ndandaro na maeneo mengine yanayoizunguka kata
hiyo, ili kuibua fursa za kiuchumi.
Kipija aliongeza vile vile wamekuwa wakiendelea na ujenzi wa
barabara mbalimbali, wilayani humo kupitia fedha zinazotengwa katika bajeti ya
halmashauri hiyo.
0 comments:
Post a Comment