Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea Jumamosi (Machi 16, 2013) kwa mechi
tatu zitakazochezwa katika miji ya Mwanza, Dar es Salaam na Manungu,
Turiani mkoani Morogoro.
Toto Africans inayopigana kukwepa
kurudi daraja la kwanza itakuwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kutoka
Tanga katika mechi itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Vinara wa ligi hiyo Yanga
wataumana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa
Manungu utakuwa mwenyeji wa mechi ya Mtibwa Sugar na Coastal Union.
UCHAGUZI TAFCA KUFANYIKA MOROGORO
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha
Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) utafanyika Jumamosi (Machi 16
mwaka huu) mjini Dodoma ambapo wajumbe wanatakiwa kuripoti siku moja
kabla ya uchaguzi.
Wagombea waliopitishwa kuwania
uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA chini ya uenyekiti wa Ramadhan
Mambosasa ni Oscar Don Koroso (Mwenyekiti), Lister Manyara (Makamu
Mwenyekiti) na Katibu (Michael Bundala).
Wengine ni Gabriel Gunda (Katibu
Msaidizi), Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania- TFF (Wilfred Kidao) wakati wagombea ujumbe wa Kamati ya
Utendaji ni Jemedali Saidi, George Komba na Magoma Rugora.
KIM KUTAJA KIKOSI CHA KUIKABILI MOROCCO
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya
Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen anatarajia kesho (Machi 13 mwaka
huu) kutaja kikosi chake kitakachoivaa Morocco.
Mkutano huo wa Waandishi wa Habari
utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
itacheza na Morocco kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Machi 24
mwaka huu.
MECHI YA SIMBA, COASTAL YAINGIZA MIL 37/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati
ya Simba na Coastal Union iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam imeingiza sh. 36,820,000 kutoka na watazamaji 6,284.
Viingilio katika mechi hiyo namba
138 iliyomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 vilikuwa
sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata
mgawo wa sh. 8,265,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 5,616,610.17.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 4,202,924.97, tiketi sh. 3,183,890, gharama za
mechi sh. 2,521,754.98, Kamati ya Ligi sh. 2,521,754.98, Mfuko wa
Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,260,877.49 na Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 980,682.49.
0 comments:
Post a Comment