Kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo, linaloshutumiwa kuzusha vurugu mashariki mwa nchi hiyo,
limesema limebadili jina la tawi lake la kijeshi na linajiandaa kuzima
mashambulio mapya dhidi yake.
Kwa
mujibu wa Kiongozi wa kundi hilo Jean-marie Runiga, sasa tawi la kijeshi la
kundi hilo litajulikana kama Jeshi la Kimapinduzi la Kongo (ARC). Katika
mahojiano na mwandishi wetu wa Goma, Runiga pia amesema kamanda wa jeshi
hilo Kanali Makenga Sultani amepandishwa cheo kuwa Jenerali.
Jumuiya
za haki za binaadamu zinalishutumu kundi la M23 kwa kuwabaka wanawake na
wasichana pamoja na kufanya mauaji wakati likipigana na jeshi la
serikali. M23 iliundwa mwezi Mei na wapiganaji wa zamani katika kundi la waasi
wa Kitutsi ambao walijumuishwa katika jeshi la taifa, kutokana na mkataba
wa amani wa 2008. Waasi hao wanadai matakwa yao hayakutekelezwa.
Hatua
hiyo ya waasi wa M23 hata hivyo imekuja siku moja baada ya Kiongozi wake
Runiga kusema kwamba huenda mapigano yakaanza tena karibuni ikiwa
serikali itakataa kuzungumza na kundi hilo.
Nchi
jirani ya Rwanda imekuwa ikishutumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 , shutuma
ambazo viongozi wa Rwanda wamezikanusha vikali.
Kwa
upande mwingine baada ya ripoti ya tume ya wataalamu wa Umoja wa mataifa
kumhusisha moja kwa moja waziri wa ulinzi wa Rwanda Jenerali James
Kabarebe kuwa ndiye mwenye kuliamrisha kundi hilo , hivi karibuni ripoti
nyingine ya Umoja huo ikaitaja pia Uganda.
Ripoti
yake ilisema maafisa wa ngazi ya juu wa Uganda wameipa M23 wanajeshi na silaha
pamoja na msaada wa kiufundi. Ripoti hiyo pia imeituhumu Uganda kutoa ushauri
wa kisiasa kwa kundi hilo na kulirahisishia mahusiano ya kigeni.
0 comments:
Post a Comment