STARS KUJIPIMA KWA ETHIOPIA JANUARI 11
Timu ya Taifa (Taifa Stars)
itacheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Ethiopia. Mechi hiyo itachezwa
Januari 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Addis Ababa,
Ethiopia.
Stars chini ya Kocha Mkuu Kim
Poulsen inatarajia kuingia kambini jijini Dar es Salaam keshokutwa
(Januari 6 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo. Mechi hiyo itakuwa
kipimo cha mwisho kwa Ethiopia kabla ya kwenda Afrika Kusini kwenye
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Januari 19
mwaka huu.
Ethiopia iko kundi C pamoja na
mabingwa watetezi Zambia, Nigeria na Burkina Faso. Ethiopia itacheza
mechi yake ya kwanza Januari 21 mwaka huu dhidi ya Zambia.
Katika mechi yake ya mwisho,
Taifa Stars iliifunga Zambia bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki
uliofanyika Desemba 22 mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya kirafiki dhidi ya
Ethiopia ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo dhidi ya Morocco
kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014. Mechi hiyo
itachezwa Machi mwaka huu.
Wachezaji wanaotakiwa kambini ni
Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula
na Mwadini Ally wote kutoka Azam. Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir
Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin
Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam),
Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank
Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco
(Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-
DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa
TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wakati benchi la Ufundi lina Kim,
Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa),
Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank
Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
UCHAGUZI KWA WANACHAMA WA TFF
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
inatarajia kukutana leo mchana (Januari 4 mwaka huu) ambapo pamoja na
mambo mengine itapitia maendeleo ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF
ikiwemo Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wanachama wa TFF (vyama vya
mikoa) wote wameshafanya uchaguzi ukiondoa mikoa ya Rukwa na Katavi
inayotarajiwa kufanya uchaguzi baadaye mwezi huu. Kwa upande wa vyama
shiriki ambavyo bado havijafanya uchaguzi ni Makocha (TAFCA), Wachezaji
(SPUTANZA), Waamuzi (FRAT) na Tiba ya Michezo (TASMA).
Vilevile Kamati ya Uchaguzi ya
TFF baada ya kikao hicho huenda ikatangaza rasmi mchakato wa uchaguzi wa
TFF unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment